Mmoja afariki, 45 walazwa kwa kunywa pombe za kienyeji

Muktasari:
- Mkazi wa Kijiji cha Nambala wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, Kenneth Nzunda (58) amefariki dunia na wengine 45 kulazwa hospitalini baada ya kunywa pombe za kienyeji.
Mbozi. Mkazi wa Kijiji cha Nambala wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, Kenneth Nzunda (58) amefariki dunia na wengine 45 kulazwa hospitalini baada ya kunywa pombe za kienyeji.
Mganga mfawidhi wa hospitali ya Serikali wilayani Mbozi (Vwawa), Dk Kenneth Lesilwa amesema wagonjwa 45 walipokewa jana katika hospitali hiyo wakiwa wanasumbuliwa na tatizo la kuharisha, kutapika na tumbo kuuma na kati ya hao wagonjwa watano walitibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Amesema pia hospitali ilipokea mwili wa mtu mmoja mwanaume aitwaye Kenneth Nzunda ambaye inadaiwa kuwa ndiye aliyekuwa akiuza pombe hiyo waliyokunywa waathirika hao.
"Kati ya wagonjwa hao kulikuwa na watoto wawili wenye umri chini ya miaka mitano, ambapo mmoja ana umri wa mwaka 1 na miezi 9 na mwingine ana umri wa miaka 2 na mwezi mmoja ambao nao wanadaiwa kunywa pombe iliyopikwa nyumbani mwao," amesema Dk Lesilwe.
Dk Lesilwe amesema miongoni mwao ni wanawake 36 na wanaume 4, lakini pia wagonjwa wengine 8 wanadaiwa kupelekwa hospitali binafsi za Ilasi Hospitali na kituo cha Afya Sifika.
"Sampuli za wagonjwa wote zimechukuliwa Ili kufanyiwa vipimo zaidi kwa kuhofia kuwa unaweza kuwa ugonjwa wa kipindupindu ambao umeingia nchini Malawi, licha ya kuwa hakuna dalili za kipindupindu," amesema Mganga huyo.
Hata hivyo Mganga huyo amesema wagonjwa 36 wanatarajia kuruhusiwa kutoka hospitalini hapo baada ya hali zao kuendelea vizuri, na wagonjwa wanne wataendelea kubaki Ili kutazamiwa zaidi
Mmoja wa wagonjwa waliolazwa katika hospitali ya Vwawa, Juliana Tuya ameeleza kuwa tukio hilo lilitokea Jumanne Oktoba 25, mwaka huu walitoka msibani baada ya mazishi walipita kilabuni wakanywa pombe na baada ya kuinywa muda mfupi walianza kusikia maumivu makali ya tumbo kisha kutapika na kuharisha.
Naye mwanamke aliyepika pombe hiyo Wema Mwampashe (40) amesema amekuwa akiendesha maisha yake kwa kupika pombe lakini anashangaa pombe aliyoipika Oktoba 25 mwaka huu kuleta madhara kwake na kwa familia yake.
"Huwa napika pombe na mume wangu ambaye anaendesha klabu ya pombe ndiye mteja wangu huniuzia na kuniletea fedha, lakini siku hiyo nilipoanza kuumwa nilimpigia simu kumueleza hali yangu na watoto wawili akiwemo na mama yangu lakini nilishangaa baadaye hakunitafuta tena hadi tulipoletwa hospitalini ndiyo nimeambiwa kafariki," amesema Wema.
Kamanda wa Polisi Mkoani hapa, ACP Alex Mukama amethibitisha kutokea tukio hilo na kwamba uchunguzi zaidi unaendelea kufanywa.