Mnyeti ‘awachana’ maafisa uvuvi

Muktasari:

  • Mnyeti amesema hayo Novemba 16, 2023 wakati amekabidhi boti mbili za kisasa kwa Chama cha Ushirika cha Wavuvi na Masoko cha Nankanga, ambzo ni sehemu ya mkopo unaotolewa kwa wavuvi kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB).

Rukwa.  Naibu Waziri wa maendeleo ya mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti amekemea tabia ya baadhi ya maofisa Uvuvi kugeuka kuwa wakusanya mapato wa halmashauri akisema hiyo siyo kazi yao, huku akiwataka kusimamia sera za uvuvi ili kuleta tija.

Mnyeti amesema hayo Novemba 16, 2023 wakati amekabidhi boti mbili za kisasa kwa Chama cha Ushirika cha Wavuvi na Masoko cha Nankanga, ambzo ni sehemu ya mkopo unaotolewa kwa wavuvi kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB).

"Kazi ya kukusanya mapato kwenye halmashauri sio ya maofisa uvuvi, nyie jikiteni kuelimisha wavuvi kuhusu matumizi ya zana bora za kisasa za uvuvi na fursa nyinginezo zilizopo kwenye sekta hiyo ili uvuvi ulete tija na mvuvi atembee kifua mbele,” amesema na kuongeza;

“Lengo la Serikali ni kuona uvuvi ulio na tija, sio kugombana sio kurumbana au kuchomeana nyavu......tendeni haki kwa wavuvi kabla ya kuwakamata na kuchoma nyavu zao au kuwapiga faini, wapeni elimu, wengine hawajui nyavu haramu ni zipi na zisizotakiwa au zinazoruhusiwa ni zipi!" amesema.

Ametaka udhibiti wa nyavu haramu za uvuvi uanzie katika viwanda na maduka yanayouza vifaa vya uvuvi visivyoruhusiwa kisheria.

Pia, Mnyeti amewataka wavuvi kuachana na vitendo vya uvuvi haramu na kuwataka kutumia vifaa vya kisasa na halali katika shughuli zao za uvuvi ili kuongeza tija na kuinua kipato chao.

“Acheni uvuvi haramu, tumieni zana za kisasa na Serikali ina na mpango madhubuti wa kuwawezesha wavuvi kupitia mradi wa boti za kisasa wenye thamani zaidi ya Sh1.5 bilioni ambao utajenga na kusambaza zaidi ya boti za kisasa 100 katika mialo ya uvuvi maeneo mbalimbali nchini,” amedokeza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuiimarisha sekta ya uvuvi kwa kukopesha vifaa vya kisasa.

Imeelezwa kuwa boti hizo zina vifaa vya kisasa vitavyorahisisha zaidi uvuvi hali itakayosaidia kuongezeka kwa mapato ya Serikali.