Mnyika: Tulijua Nyalandu na Mathew wataondoka

Mnyika: Tulijua Nyalandu na Mathew wataondoka

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema chama hicho kilifahamu kuwa Lazaro Nyalandu na Seleman Mathew, ambao wote walikuwa wajumbe wa kamati kuu ya chama hicho, wangeondoka kutokana na mienendo yao waliyokuwa wakiionyesha kwa hivi karibuni.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema chama hicho kilifahamu kuwa Lazaro Nyalandu na Seleman Mathew, ambao wote walikuwa wajumbe wa kamati kuu ya chama hicho, wangeondoka kutokana na mienendo yao waliyokuwa wakiionyesha kwa hivi karibuni.

“Hawa ni wasaliti, wamejiongeza wameshindwa kuvumilia baada ya mateso ya kuporwa ushindi wa ubunge mwaka 2020. Chadema itasonga mbele hadi mabadiliko, uhuru na haki na demokrasia vipatikane nchini.

“Mapengo yao yatazibwa na makamanda wengine na mapambano yanaendelea,” alisema Mnyika bila kutaka kufafanua kwa kina.

Juzi CCM iliwapokea Nyalandu na Mathew ambao ni makada wake wa zamani waliokihama chama hicho kati ya mwaka 2015 na 2017 na kwenda Chadema ambako hivi karibuni Nyalandu alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kanda ya Kati na Mathew kuwa Mwenyekiti wa Kanda ya Kusini.

Wawili hao walitangaza uamuzi huo katika mkutano mkuu maalumu wa CCM jijini Dodoma mbele ya Mwenyekiti mpya wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan, huku wakiweka bayana masaibu waliyopitia na uamuzi wao huo wa kurejea kwenye chama tawala.

Nyalandu, aliyekuwa wa pili kutambulishwa na Rais Samia aliikana ahadi yake kutoihama Chadema ikiwa zimepita siku 1,278 tangu alipojiondoa CCM.

Kwa nyakati tofauti, Nyalandu amekuwa akijinasibu kuwa hawezi kuihama Chadema, kwa mara ya kwanza alimtaka Machi mwaka 2019 akisema yeye hakwenda Chadema kwa mafuriko. Msingi wa kauli ulitokana na kitendo cha Edward Lowassa kurejea CCM akitokea Chadema.

Kama hiyo haitoshi, Nyalandu alirejea kauli hiyo Agosti 2020 kwa staili tofauti katika mkutano mkuu wa Chadema wa kuchagua jina moja la mgombea urais aliyepeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu uliopita.

Katika mkutano huo, Nyalandu alishindwa na mpinzani wake, Tundu Lissu na baada ya matokeo kutangazwa aliwaondoa hofu wanachama wa Chadema kuhusu mapenzi yake ndani ya chama hicho, akisisitiza yupo pamoja nao.

Lakini, jana katika mkutano mkuu wa CCM akitumia staili ya kunukuu baadhi ya vifungu vya biblia Nyalandu alisema: “Hakuna furaha izidiyo furaha ya mtoto arejeapo nyumbani.

“Wimbo wa bwana hauimbiki katika nchi ya ugenini, Mzee Sumaye (Frederick), Lowassa (Edward) na Dk Slaa (Wilbroad) ni mashuhuda wachache kati ya wengi kwa nini wimbo wa bwana hauimbiki katika nchi ya ugenini. Nakupongeza Rais kwa uongozi wako shupavu, nakushukuru kwa kukubali kunipokea na kunisamehe pamoja na kuniruhusu kurejea chamani,” alisema Nyalandu ambaye ni wazari wa zamani wa Maliasili na Utalii.

Kwa upande wake, Mathew alisema: ‘‘Nimekuja hapa kusema neno moja, nimeamua kurudi nyumbani. Nilikuwa ndani ya CCM na niliondoka CCM. Lakini, kadri unavyoendelea kuwa nje ya Chama cha Mapinduzi basi unajihisi una upungufu, leo (jana) nina furaha kubwa ya kuja mbele yenu wajumbe wa mkutano mkuu na kamati kuu,” alisema Mathew, maarufu ‘Messi’ aliyewahi kuingia kwenye mikwaruzano na mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye kwenye uchaguzi wa mwaka 2015 na 2020.

Sio katika uchaguzi mkuu tu, bali hata kwenye kura za maoni ndani ya CCM za mwaka 2015 ambazo Nape pia alimshinda Messi. Hatua hiyo ilizua sintofahamu na kuamua kutoka CCM kuhamia Chadema.