Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mpango atoa neno uwekezaji kutumia fedha za mifuko ya hifadhi

New Content Item (1)

Muktasari:

  • Imeelezwa uwekezaji kupitia mifuko ya hifadhi ya jamii unaweza kuathiri lengo la msingi la mifuko husika la kutoa ulinzi wa kijamii hasa kwa wastaafu, wagonjwa na watu wenye ulemavu, iwapo hakutafanyika upembuzi thabiti kabla ya uwekezaji.

Arusha. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amezishauri nchi za Afrika zinapowekeza kwenye miradi ya miundombinu kupitia mifuko ya hifadhi ya jamii, kuwekeza kwenye miradi inayotekelezeka ambayo haitadhoofisha uwezo wa mifuko hiyo na kuathiri malengo ya kuanzishwa kwake.

Dk Mpango ameyasema hayo leo Alhamisi Julai 10, 2025 jijini Arusha, alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika kongamano la 14 la watunga sera wa sekta ya hifadhi ya jamii barani Afrika.

Amesema uwekezaji wa mifuko hiyo katika maendeleo ya miundombinu ya kijamii na kiuchumi, imegubikwa changamoto mbalimbali, hivyo tahadhari ni muhimu kuchukuliwa kabla ya uwekezaji.

Amesema kutokana na hatari hizo ni lazima wahakikishe miradi ya miundombinu ambayo inawekezwa na mifuko hiyo inakuwa na uwezo wa kiuchumi, inayotekelezeka ili isiathiri na kudhoofisha uwezo wa mifuko hiyo kutimiza wajibu wake.

“Iwapo upembuzi yakinifu wa miradi hiyo ya miundombinu hautafanywa mapema inaweza kusababisha muda mrefu wa malipo kwa walengwa au hata kushindwa kabisa kuwalipa,” amesema.

“Tahadhari ichukuliwe ili kuepusha miradi iliyopangwa vibaya na yenye gharama kubwa na migumu kupita kiasi ambayo ni ngumu kuisimamia na ile isiyoshughulikia mahitaji ya walengwa wa mifuko ya hifadhi ya jamii,” ameongeza.

Amesema mabadiliko yanaonyesha kuwa sekta isiyo rasmi barani Afrika inachukua asilimia kati ya 40 hadi 60 ya uchumi na maendeleo ya miundombinu ni duni sana hasa vijijini, na kuwa wataalamu wanapaswa kuja na suluhisho ili kuongeza tija na ubora wa maisha katika maeneo ya pembezoni.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Dk Mpango amesema kwa upande wa Tanzania, mifuko hiyo imekuwa na mchango mkubwa kuongeza juhudi za Serikali kwa miaka mingi kwenye ujenzi wa miundombinu ya kijamii na kiuchumi na kuwa miradi hiyo inahitajika barani Afrika.

“Kwa mfano, imeshiriki katika kufadhili miradi kadhaa ikijumuisha nyumba za makazi na biashara zikiwamo za Garden Avenue Tower, Sam Nujoma Commercial Complex, Dege Eco Village, Dungu Farm, viwanda vya ngozi, sukari, pamba na chai,” amesema.

Amesema nchi za Afrika zinakadiriwa kuwa na upungufu wa ufadhili kati ya Dola za Marekani 68 bilioni hadi 108 bilioni kwa mwaka, huku upungufu wa miundombinu ukikadiriwa kila mwaka kuhitajika kati ya Dola za Marekani 130 bilioni hadi 170 bilioni.

Amesema mifuko hiyo  barani humo inatajwa kuwa mbadala sahihi katika kuchochea ujenzi wa miundombinu ya maendeleo na kuwataka watalaam walioshiriki kikao hicho, kutoka na mikakati ya jinsi mifuko hiyo inavyoweza kuchangia katika kuongeza ufadhili wa uwekezaji.

Awali, Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete amesema kongamano hilo lililoandaliwa na wadau wa sekta ya hifadhi ya jamii Afrika (ASSA), limelenga kukutanisha wadau, watunga sera, wasimamizi na watendaji wa sekta hiyo.

“Kupitia kongamano hili tutaangalia mapungufu ya kisera ili kukuza ukuaji wa uchumi wa maendeleo endelevu barani Afrika hasa tukiangalia miundombinu kama kichocheo cha maendeleo na ukuaji wa uchumi,”amesema.

“Kutokana na migogoro au vita zinazoendelea maeneo mbalimbali duniani zimevuruga hali ya biashara na kufanya nchi nyingi hasa za Afrika ambazo zilikuwa zinategemea misaada kutoka nje kushindwa kujiendesha.”

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa ASSA, Meshach Bandawe amesema kongamano hilo limehudhuriwa na nchi wanachama zikiwamo  Tanzania, Kenya, Uganda, Zambia, Zimbabwe, Sierra Leone, Rwanda, Burundi, Malawi, Comoro, Sudan Kusini, Mali, Namibia, Ghana, Afrika Kusini, DRC, Nigeria, Cote d’Ivoire na Gambia.

Mwenyekiti wa ASSA, Muyangwa Muyangwa amesema nchi za Afrika zinapiga hatua kubwa katika kujenga misingi mizuri ya mifumo ya mifuko hiyo kwa ujumuishaji wa makundi mbalimbali.

“Kongamano la mwaka huu linashirikisha wazungumzaji watakaowasilisha mada zitakazoangalia nini kifanyike kila mmoja kwa nafasi yake kuanzia watunga sera, wawekezaji na wadau wengine,” amesema.