Mpanju ajivunia utendaji wa RITA

New Content Item (2)
New Content Item (2)

Muktasari:

Kwa sasa RITA imekuwa mkombozi kwenye utunzaji wa taarifa za matukio muhimu kutokana na kuboreshwa kwa mifumo yake.

TANZANIA imetajwa kama nchi ya mfano kwa Ukanda wa Kusini mwa jangwa la Sahara kutokana na kufanya vizuri kwenye usajili ya matukio muhimu ikiwemo vizazi, vifo, ndoa na talaka kwa ufanisi.
Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju wakati akizungumza na watumishi wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), ambapo amesema jitihada na uwajibikaji ndio umeifanya Tanzania kuwa kinara.
Amesema mataifa mengine Afrika yanaitazama Tanzania kama mfano wa kuigwa kwenye kurekodi na kutunza taarifa muhimu kuhusu wananchi wake.
Mpanju alitoa pongezi hizo jana wakati akifungua kikao cha 23 cha Baraza la Wafanyakazi wa RITA kilichofanyika jijini Arusha.
“Kazi ni nzuri na mataifa mengine yanataka kujifunza kwetu, tayari Ethiopia wameanza kutekeleza mkakati wa usajili wa matukio muhimu na takwimu baada ya kujifunza kwetu. Tunajivunia sifa hiyo na hilo linadhihirisha kwamba, kazi inayofanyika pale RITA ni ya uhakika na ina tija kwa maendeleo ya Taifa,” alisema Mpanju.
Naye Mwenyekiti wa baraza hilo ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa RITA, Emmy Hudson alisema juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali katika kuboresha mifumo ya usajili na maboresho ya sheria vimekuwa na tija kubwa kwa Wakala.
"Tumefanikiwa kuwapokea majirani zetu kutoka Uganda waliyokuja kujifunza kuhusu masuala ya usajili wa vizazi, vifo, ndoa na talaka, na kama nchi tumejipanga kuendelea kuboresha mifumo ili kwenda na wakati,” alisema Emmy.