Mradi wa bomba la mafuta kuanza Aprili mwaka huu

Mradi wa bomba la mafuta kuanza Aprili mwaka huu

Muktasari:

  • Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani amewataka Watanzania kuchangamkia fursa zinazotokana na mradi wa ujenzi wa Bomba la Mafuta Hoima nchini Uganda hadi Tanga nchini Tanzania utaanza Aprili mwaka huu na kukamilika baada ya miaka mitatu.

Dodoma. Waziri wa Nishati Dk Medard  Kalemani amewataka Watanzania kuchangamkia fursa zinazotokana na mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta Hoima nchini Uganda hadi Tanga nchini Tanzania, akisema mradi huo utaanza kujengwa Aprili mwaka huu na kukamilika baada ya miaka mitatu.


Dk Kalemani ameyasema hayo leo Jumatatu Aprili 12 2021 wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kiteto (CCM) Edward Ole Lekaita.


Mbunge huyo alitaka kufahamu iwapo serikali iko tayari kutoa kipaumbele katika ajira na fursa zinazotokana na mradi huo.
Akijibu swali hilo, Dk Kalemani mradi huo ni mkubwa na utapita katika mikoa minane, wilaya 24, vijiji 127 na vitongozi 502 na utatoa ajira zaidi 10,000 katika hatua za awali na hadi 15,000 katika hatua za ujenzi.


Amewaomba wakazi wa maeneo ambayo mradi huo utapita wajitokeze kuchuklua fursa kwasababu zimeziweka kwa ajili ya watanzania.


Katika swali la msingi, Ole Lekaita amehoji mkakati gani wa kutoa ajira za upendeleo kwa vijana na fursa nyingine za kibiashara kwa wananchi wa Jimbo la Kiteto kupitia mradi mkubwa wa kimkakati wa bomba la mafuta (Hoima – Bandari ya Tanga) ambalo linapitia katika Wilaya ya Kiteto.


Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Nishati Stephen Byabato amesema Wilaya ya Kiteto itapitiwa na bomba kwa urefu wa kilomita 117.1 pamoja na ujenzi wa kambi ya kuhifadhi mabomba katika kijiji cha Ndaleta na kambi ya wafanyakazi katika Kijiji cha Njoro.


Amesema kutokana na Bomba hilo kupita katika Wilaya ya Kiteto, wananchi wa Kiteto wanufaika na ujenzi wa mradi huo kwa kufanya biashara, ajira na fursa za kiuchumi na kijamii.
Amesema utekelezaji wa kazi za mradi huu unatarajiwa kuanza Aprili mwaka huu na kukamilika mwezi Julai, 2023.


Amesema Serikali kupitia Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na wadau wengine inaendelea kutoa hamasa ili wananchi wanufaike na shughuli za ujenzi na uendeshaji wa mradi.