Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mradi wa maji utakavyowanufaisha wananchi Serengeti

Ofisi ya Kata ya Nyansurura wilayani Serengeti iliyozinduliwa na mbio za mwenge. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

  • Baada ya kukamilika kwa mradi huo upatikanaji wa maji kijijini hapo umefikia asilimia 100 kutoka asilimia tano za mwanzo huku wakazi wote 2,646 wakinufaika.

Serengeti. Wakazi wa Kijiji cha Nyamihuru wilayani Serengeti, Mkoa wa Mara, wameondokana na adha ya ukosefu wa maji baada ya kukamilika kwa mradi wa maji safi na salama uliogharimu zaidi ya Sh572.5 milioni.

Awali, hali ya upatikanaji wa maji kijijini humo ilikuwa asilimia tano pekee, lakini baada ya kukamilika kwa mradi huo Novemba 2024, huduma imefikia asilimia 100 na kunufaisha wakazi wote 2,646.

Meneja wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) Wilaya ya Serengeti, Deus Mchele, amesema wananchi walichangia zaidi ya Sh5.2 milioni kwa kutoa ardhi bila fidia ili kurahisisha utekelezaji wa mradi huo.

“Wananchi walikuwa wakichota maji machafu milimani, wakishindana na fisi na ngedere. Sasa upatikanaji wa maji safi na salama umefikia asilimia 100 na changamoto hiyo imekwisha,” amesema.

Baadhi ya wakazi wamesema kabla ya mradi walilazimika kutembea zaidi ya kilomita 10 kutafuta maji, hali iliyosababisha kupoteza muda na nguvu za kushiriki shughuli za maendeleo.

“Kule mlimani ni zaidi ya kilomita tano kutoka hapa. Ukirudi na ndoo moja ya maji, tayari umechoka, huna nguvu za kwenda shambani,” amesema mkazi Annasatazia Ghati.

Akizindua mradi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Ismail Ussi, amesema serikali imeweka mkakati wa kudumu kutatua kero ya maji, ikiwemo programu ya uchimbaji wa visima 900 nchi nzima.

“Kilio cha maji kilikuwa ni kubwa hasa vijijini. Serikali imeamua kwa dhati kuhakikisha wananchi wanapata huduma hii muhimu kwa maisha ya binadamu na viumbe hai,” amesema.

Katika hatua nyingine, Ussi amezindua jengo jipya la Ofisi ya Kata ya Nyansurura lililogharimu Sh90 milioni kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Serengeti. Jengo hilo litahudumia wakazi 10,760 wa kata hiyo.

Amewataka wananchi kulitumia jengo hilo kwa masuala ya maendeleo badala ya migogoro ya kifamilia au kijirani.

Wakati huohuo, wanafunzi wa Kijiji cha Nyamihuru wameondokana na adha ya kutembea zaidi ya kilomita 20 kwenda na kurudi shule baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Shule ya Sekondari Kebaroti.

Shule hiyo, iliyogharimu Sh670.2 milioni, imewaondolea wanafunzi mzigo wa kusoma mbali katika Sekondari ya Busawe ambayo ni ya kata.