Msajili aitisha mkutano kujadili mvutano kati ya polisi, vyama vya siasa

Msajili aitisha mkutano kujadili mvutano kati ya polisi, vyama vya siasa

Muktasari:

  • Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amesema ofisi yake inafanya jitihada za kuwa na mkutano wa wadau wa siasa siku chache zijazo ili kujadili na kuondoa mvutano kati ya vyama vya siasa na jeshi la polisi.

Dar es Salaam. Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amesema ofisi yake inafanya jitihada za kuwa na mkutano wa wadau wa siasa siku chache zijazo ili kujadili na kuondoa mvutano kati ya vyama vya siasa na jeshi la polisi.


Akizungumza na vyombo vya habari leo Jumatatu Septemba 6, 2021 jijini Dar es Salaam, Jaji Mutungi amesema mkutano huo utahusisha wadau watatu muhimu ambao ni jeshi la polisi, vyama vya siasa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.


Amesema aliwasiliana na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro wakakubaliana kukutana na wadau hao hivi karibuni kwa lengo la kujadili suala la mvutano baina ya polisi na vyama vya siasa.


"Imekuwa kila mkutano vya vyama vya siasa tunaona askari wamejazana, this is not a military state (hii siyo nchi ya kijeshi). Tumeliona hilo, tukasema tuwaite wadau tujadili.


"Sitarajii kuona vyama vya siasa vikiendelea na hiyo mikutano yao wakati jitihada hizi zinafanyika," amesema Jaji Mutungi akisisitiza vyama vya siasa kuwa na subira.


Amesema katika mkutano huo, wanataka kuondoa kitu ambacho polisi wanadhani vyama vya siasa vinakosea na kile ambacho vyama vya siasa vinadhani polisi wanakosea.


Hivi karibuni, jeshi la polisi limeingia kwenye mvutano na Chama Cha NCCR Mageuzi baada ya kuzuia kikao cha kamati kuu kilichokuwa kifanyike Agosti 28 mwaka huu katika ukumbi wa Msimbazi Centre kwa madai kwamba kulikuwa na viashiria vya uvunjifu wa amani.