Msako JAB wahamia mikoani, wahariri wataka maboresho ya taaluma
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Patrick Kipangula, akizungumza na waandishi wa habari.
Muktasari:
- JAB imeanza utekelezaji wa utaratibu huo ili kutambua mchango wa wanahabari walioitumikia kwa muda mrefu na kwa weledi taaluma ya habari nchini
Dar es Salaam. Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imezindua rasmi utaratibu wa kutoa ithibati ya uanachama wa maisha kwa wanahabari wakongwe waliokuwa na umri wa miaka 50 na kuendelea.
Hatua hiyo inatekelezwa kwa kuzingatia mwongozo wa kisheria unaowapa sifa ya kupata hadhi hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa JAB, Tido Mhando kwenye kongamano lililofanyika leo Jumamosi 11, 2026 katika Maonyesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Mhando amesema bodi imeanza utekelezaji wa utaratibu huo ili kutambua mchango wa wanahabari walioitumikia kwa muda mrefu na kwa weledi taaluma ya habari nchini.
Amesema uanachama wa maisha ni sehemu ya juhudi za kuthamini na kuheshimu mchango wa wanahabari wakongwe, sambamba na kutekeleza matakwa ya sheria na miongozo inayosimamia ithibati ya taaluma ya uandishi wa habari.
Kaimu Mkurugenzi wa JAB, Patrick Kipangula amesema bodi hiyo imeanza ukaguzi wa mkoa kwa mkoa ili kuhakikisha kila mwandishi anayefanya kazi kwenye sekta ya habari anatimiza masharti ya kitaaluma na yaliyowekwa na sheria.
“Tunataka kujiridhisha kwamba watu wanaofanya kazi katika tasnia ya habari wana sifa na vigezo vinavyotakiwa kisheria. Kila mtu anayejihusisha na uandishi wa habari kwa sasa lazima akidhi masharti hayo.
“Kuna mambo mengi yanayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, lakini maamuzi ya ithibati yanategemea uhakiki. Kama mtu hana sifa zinazotakiwa, hawezi kurejea kwenye utangazaji au uandishi wa habari hadi atakapokidhi masharti hayo,” amesema.
Mhariri wa Mwananchi, Lilian Timbuka amesema sekta ya habari inahitaji mageuzi ili kurejesha weledi na kuimarisha ubora wa kazi za uandishi wa habari.
“Tunahitaji kuona mabadiliko. Kila kona ya nchi inapaswa kuwa na waandishi wenye uwezo na wanaokidhi viwango vinavyotakiwa. Njia za mkato na utendaji usio wa kitaaluma unaoonekana sasa lazima ukome,” amesema.
Pia, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha uchumi wa vyombo vya habari, akisema sekta yenye uwezo wa kifedha ni muhimu katika kuendeleza uwajibikaji na maendeleo ya taifa.
Mhariri Mtendaji wa Nipashe, Salome Kitomari amesema changamoto za kifedha zimeathiri kwa kiasi kikubwa uandishi wa habari za uchunguzi, huku vyombo vingi vikishindwa kugharamia safari za waandishi kwenda kufuatilia taarifa kwa kina.
“Leo vyombo vingi vya habari haviwezi kumudu uandishi wa uchunguzi. Ukimtuma mwandishi kwenda mkoa mwingine kufuatilia taarifa, lazima kuwe na rasilimali za kuwezesha kazi hiyo,” amesema.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema kuboresha taaluma ya habari kunahitaji mfumo imara wa ulezi wa kitaaluma na kuimarisha mifumo ya kujisimamia, ikiwamo kuanzishwa kwa baraza huru la kushughulikia malalamiko ya sekta.
Pia, amesema uzoefu unapaswa pia kutambuliwa sambamba na sifa za kitaaluma, hasa kwa wanahabari wakongwe waliotumikia kwa miongo kadhaa katika vyumba vya habari.
“Kuna waandishi ambao wamekuwa kwenye vyumba vya habari tangu mwaka 1989. Huwezi kuwaambia leo warudi darasani kuanza kusoma stashahada. Wana maarifa na wanaweza kuwa walimu wa kizazi kipya cha waandishi,” amesema.
Mhariri wa Media Brains, Jesse Kwayu amesema waandishi wanahitaji kupewa mazingira bora zaidi ya kufanya kazi, hususan katika uandishi wa habari za uchunguzi.
“Majukwaa ya kidijitali yamefungua fursa mpya. Waandishi sasa wanaweza kufika maeneo ambayo hapo awali yalikuwa magumu kuyafikia. Tunapaswa kutumia teknolojia kuongeza uwajibikaji, ufanisi na tija katika kazi yetu,” amesema.