Mshtakiwa aomba akutanishwe na mkewe aliye mahabusu wajadili hatima ya watoto

Mshtakiwa Najim Mohamed, anayekabiliwa na mashtaka mawili ya kusafirisha dawa za kulevya zenye uzito wa kilo 3,050 akiwa chini wa ulinzi wa askari Magereza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Wawili hao wanashtakiwa wakidaiwa kusafirisha dawa za kulevya.

Dar es Salaam. Mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya kusafirisha kilo 3,050 za dawa za kulevya, Najim Mohamed ameiomba Mahakama imkutanishe na mke wake wajadiliane juu ya hatima ya shule ya watoto wao.

Mohamed (52), mkewe Maryam Najim (50) na mfanyakazi wa ndani, Juma Abbas (37), wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi wakishtakiwa kwa makosa mawili ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini na methamphetamine.

Mohamed ametoa ombi hilo leo Mei 15, 2024, mbele ya Hakimu Mkazi Aaron Lyamuya katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Amewasilisha ombi hilo muda mfupi baada ya Wakili wa Serikali, Eva Kassa kudai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika. Kesi hiyo imeendeshwa kwa njia ya video.

Mohamed alinyoosha mkono kuomba kuzungumza.

Hakimu alimuuliza ana shida? Alijibu ndiyo. Hakimu akampa nafasi ya kuzungumza.

Alipopewa nafasi amesema: "Naomba Mahakama yako inikutanishe na mke wangu niweze kujadiliana naye mambo ya kifamilia kwa sababu watoto wetu wanatakiwa kwenda shule na sisi tupo mahabusu."

Hakimu Lyamuya alimuuliza anajua sababu ya yeye na mke wake kutengenishwa mahabusu?

Mohamed akajibu anajua sababu za kutenganishwa.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Lyamuya amesema ombi la mshtakiwa limechukuliwa na atapewa majibu tarehe nyingine kesi itakapotajwa.

Hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 27, 2024 itakapotajwa tena. Washtakiwa wameendelea kubaki rumande kutokana kesi inayowakabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Mara ya kwanza washtakiwa walifikishwa mahakamani hapo, Desemba 29, 2023 na kusomewa mashtaka ya uhujumu uchumi.

Katika shtaka la kwanza, kwa pamoja wanadaiwa Desemba 15, 2023 katika eneo la Kibugumo Shule lililopo wilayani Kigamboni, walisafirisha heroini yenye uzito wa kilo 882.71.

Katika shtaka la pili, wanadaiwa siku na eneo hilo, kwa pamoja walisafirisha Methamphetamine yenye uzito wa kilo 2,167.29.