Mshtakiwa aomba hukumu yake iahirishwe akidai akili haiko sawa

Washitakiwa Waziri Mohamed (kushoto) na Mohamed Ndumi wakifikishwa Mahakama ya Wilaya Handeni kwa ajili ya kesi inayowakabili. Picha Wilaya na Rajabu Athumani

Muktasari:

  • Washtakiwa wa kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha wameomba mahakama iahirishe kuwasomea hukumu dhidi yao wakidai hawajisikii vizuri kiafya huku mwingine akidai akili yake haiko sawa.

Handeni. Mahakama ya Wilaya ya Handeni imeahirisha kuwasomea hukumu washtakiwa wawili wa kesi ya unyang'anyi kwa kutumia silaha, Waziri Mohamedi na mwenzake Mohamed Ndumi baada ya kuieleza mahakama hiyo kuwa hawajisikii vizuri kiafya, mmoja akiomba dawa na mwingine akidai akili haiko sawa.Hukumu hiyo ilikuwa imepangwa kusomwa leo Aprili 8, 2024 na Hakimu Mkazi Veronica Siao aliyesikiliza kesi hiyo, lakini washtakiwa hao wameiomba mahakama iwapangie siku nyingine kutokana na sababu hizo za kiafya.Washtakiwa hao wametoa maelezo hayo na kuomba ahirisho hilo baada ya kuulizwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Nzagalila Kikwelele, kama walikuwa tayari kwa ajili ya kusikiliza hukumu hiyo, lakini kila mmoja kwa nyakati tofauti wakaeleza hawataweza kuisikiliza kwa kuwa wanajisikia vibaya kiafya.Mshtakiwa wa kwanza, Waziri alipoulizwa na wakili Kikwelele kama alikuwa tayari kusikiliza hukumu hiyo, alidai kuwa anajisikia vibaya baada ya kuhisi homa wakati kesi hiyo inaendelea mahakamani na kwamba alihitaji dawa ameze, hivyo akaomba kupangiwa tarehe nyingine."Mheshimiwa leo siko vizuri kiafya naomba kama inawezekana hukumu yetu ipangiwa tarehe nyingine ya kusomwa, halafu naomba nipate hata dawa nimeze kwanza kabla sijarudishwa mahabusu," amesema WaziriKwa upande wake mshtakiwa wa pili, Mohamed amesema, hataweza kusikiliza hukumu hiyo kwa kuwa akili yake haiko sawa, hivyo naye akaomba apangiwe tarehe nyingine ili kwanza ikae sawa."Mheshimiwa hakimu naomba kesi ipangiwe siku nyingine, kwani hajisikii vizuri, lakini hata kiakili sipo sawa," amesema Mohamed.Wakili Kikwelele ameunga mkono maombi yao hao akisema wana haki ya kusikilizwa, hivyo naye akapendekeza kesi hiyo isogezwe mbele mpaka Aprili 12, mwaka huu kwa ajili ya kusomewa hukumu hiyo kama watakuwa tayari.Hakimu Siao baada ya kusikiliza pande zote naye ameridhia maombi ya ahirisho la hukumu hiyo.“Kwa kuwa washtakiwa wameomba wapangiwe tarehe nyingine kwa sababu wanajisikia vibaya, basi kesi hii inaahirishwa mpaka tarehe 12, mwezi wa nne mwaka 2024 itaendaelea,” amesema Hakimu Siao.Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani hapo kwa mara ya kwanza Mei 17, 2023 kwa mshtaka ya unyang'anyi wa kutumia silaha, wakidaiwa kupora pikipiki yenye thamani ya Sh2.1 milioni katika Kijiji cha Kwankonje.