Msichana wa miaka 32 ajitosa kugombea uspika

Thursday January 13 2022
msichana

Ester Makazi baada ya kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea nafasi ya Spika wa Bunge la Tanzania

By Nasra Abdallah
By Mainda Mhando

Dar/Dodoma.

Mkazi wa Temeke, Ester Makazi amechukua fomu ya kuomba kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea nafasi ya Spika wa Bunge la Tanzania.

Ester mwenye miaka 32 amechukua fomu hiyo leo Alhamisi Januari 13, 2022 katika ofisi ndogo za CCM Lumumba jijini Dar es Salaam.

Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu hiyo, Ester amesema amejitafakari na ameona anaenea kukalia kiti hicho kwa kuwa ni binti, kijana na ana uzoefu na tayari Rais Samia Suluhu Hassam amekuwa mfano kwake kwamba wanawake wanaweza.

"Uzoefu wangu katika chama nimewahi kuwa mjumbe katika Tawi langu la Toangoma na kufanya shughuli za kichama na maendeleo hivyo nimejipima nikaona ninaweza kugombea nafasi hii," amesema Ester ambaye ni mhitimu wa shahada ya ya Sheria Chuo cha Tumaini.

Wengine waliojitokeza kuchukua fomu kwa siku ya leo ni Mohammed Mmanga, ambaye amesema amejitokeza kugombea kwa kuwa ana uzoefu wa muda mrefu katika chama kwani ameanzia chipukizi.

Advertisement

Mmanga amesema endapo atafanikiwa kuchaguliwa kuwa Spiaka anaahidi haatawangusha wabunge wala chama chake kwa kuwa uwezo anao.

Wakati mchumi na msimamizi wa masuala ya fedha, biashara, uwekezaji, Dk Godwin Maimu ambaye alikuwa miongozni mwa waliofika ofisi za Lumumba na kuchukua fomu hiyo akisema nia ya kuitaka nafasi hiyo ni kuleta mabadiliko ya uongozi ndani ya Bunge na Taifa.

“Nampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutaka kuwapo kwa mchakato wa kuwania nafasi ya uspika. Mimi kama kijana nimejikagua nikaona ninatosha na ninafaa kuwania nafasi hiyo na ndiyo maana nimefika hapa leo,” alisema Dk Maimu.


Maige naye achukua Dodoma

Katika ofisi za makao makuu ya CCM Dodoma, Aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii na Mbunge wa Msalala mkoani Shinyanga Ezekiel Maige naye amechukua fomu hizo.

Akielezea kilichomsukuma kuitaka nafasi hiyo, Maige amesema ana uzoefu katika uongozi na Bunge hilo kwa kulitumika kwa zaidi ya miaka 13.

Amesema ana historia nzuri na chama hicho kwani alijiunga akiwa na umri wa miaka 19 hivyo ana uwezo wa kukiwakilisha vema katika kuleta maendeleo ya nchi hasa katika kupambana na umaskini, ujinga na maradhi.

Amesema amejitokeza kuwania nafasi hiyo ili kutekeleza haki za kikatiba ya chama hicho zikiwemo za kuitumikia nchi na watu wake na kujitolea kwa nafsi kuondosha umaskini.

“Kupitia katiba za Chama changu wakati naingia niliahidi kama mwanachama nitatekeleza ahadi zote na nikifanikiwa katika hili naahidi kutoa ushirikiano katika Bunge hususan kwenye mambo ya sheria” amesema

Advertisement