Msimamo wa kikokotoo, fao la kujitoa

Thursday November 25 2021
msimamopic
By Sharon Sauwa

Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama amesema uamuzi kuhusu mfumo utakaotumika katika kukokotoa mafao ya wastaafu utajulikana baada ya kumalizika kwa majadiliano yanayoendelea kati ya Serikali, wafanyakazi na waajiri.

Waziri Jenista alitoa kauli hiyo Jumanne Novemba 24, 2021, wakati akielezea mafanikio ya miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara), ambapo alisisitiza kuwa mfumo mpya utaanza baada ya muda wa mpito kumalizika mwaka wa fedha 2022/23.

Alisema kikotoo cha mafao ya wastaafu ni suala jumuishi na linaloshirikisha pande tatu na taarifa ya suala hilo itatolewa kwa pamoja kwa dhana ya utatu huo.

“Taarifa itatolewa kwa pamoja kwa kuzingatia dhana ya utatu pale shughuli nzima ya kupitia huo mfumo itakapokamilika. Na kupitia mfumo ilikuwa ni pamoja na kufanya tathmini ya mifuko (shughuli) ambayo tumemaliza sasa,” alisema.

Madeni ya Mifuko ya Hifadhi

Kuhusu madeni ya mifuko ya hifadhi ya jamii, Mhagama alisema kuwa taarifa za PSSSF zinaonyesha kuwa mfuko huo unadai Sh10.6 trilioni, lakini ili Serikali iweze kulipa fedha hizo ni lazima ifanye uhakiki.

Advertisement

“Rais Samia ameagiza fedha iliyofanyiwa uhakiki ambayo ni Sh2 trilioni ilipwe kwa kutumia hati fungani ambayo mfuko sasa ukipata una uwezo wa kulipa madeni limbikizi,” alisema.

Alisema hapo awali wafanyakazi walikuwa hawachangii katika mifuko hiyo, lakini walikuwa wanalipwa pensheni na ilipofika mwaka 1999 ndio walianzisha Mfuko wa PSSSF ambao wafanyakazi wa umma walitakiwa kuchangia katika mifuko hiyo.

Alisema licha ya kutochangia katika mifuko hiyo awali, ilipofika mwaka 2004 baadhi yao walitakiwa kuanza kulipwa mafao yao na sehemu ya mafao yao wanayotakiwa kulipwa ilikuwa hawajaichangia katika mifuko hiyo.

Mhagama alisema kati ya deni hilo, Sh4.6 trilioni lilikuwa ni deni la michango ya wafanyakazi ambao hapo awali walikuwa hawachangii katika mifuko hiyo ya hifadhi ya jamii.

Kuhusu deni linalotokana na uwekezaji, Mhagama alisema hadi sasa Serikali imeshalipa Sh500 bilioni kati ya Sh700 bilioni zilizohakikiwa na kwamba wanaamini kwa mwenendo huo madeni hayo yataisha.

Kuhusu mafao ya kujitoa ambayo yameondolewa, Mhagama alisema ni eneo jingine lililofanyiwa kazi na kamati ya pamoja inayopitia mfumo wa mpito na kutengeneza hifadhi ya jamii kuwa endelevu.

“Eneo la fao la kujitoa ni eneo ambalo linafanyiwa kazi vya kutosha, lakini tumesema mifuko itaendelea kupokea maelekezo ya Serikali na ninakumbuka wakati wa Hayati Rais John Magufuli alitoa maelekezo kuona ni namna gani fao hili linaweza kulipwa kwa kuzingatia aina ya mfanyakazi anayedai fao hili,” alisema.

Alisema fao hili linawafaa sana watu ambao hawategemei kupata ajira tena baada ya kuondoka katika eneo la kazi.

Alisema mfumo wa hifadhi ya jamii ni kuwalinda Watanzania wanapokuwa kazini na wanapotoka katika mfumo wa ajira.

Waziri Mhagama alisema kwa sasa Ofisi ya Waziri Mkuu inakamilisha utekelezaji maelekezo ya Serikali ya kuimarisha mfumo wa mafao ya watumishi kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi

Mhagama alisema vikao vya kuangalia namna ya kuunganisha mamlaka za Usimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu vimeshaanza.

Kuhusu malalamiko ya vyama vya upinzani kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) haiko huru, Mhagama alisema tume hiyo ina uhuru wa kutosha na wala haiingiliwi na Serikali.

Alisema Katiba imeweka tume kuwa huru na kwamba Serikali inashughulika na Sera na bajeti.

“Hivi tunajiuliza uhuru wa Tume hii ni kitendo cha Rais kuteua Mwenyekiti wa tume, kwa sababu chaguzi sita zilizofanyika nchini zimekuwa zikisimamiwa na tume hii na uchaguzi umeisha kwa uhalali,” alisema.

Alisema baadhi ya viongozi wa upinzani wamechaguliwa kupitia tume hiyo na kuhoji mbona hawakusema wamechaguliwa na tume isiyokuwa huru kwamba hawataingia katika vyombo vya maamuzi.

Alihoji kama ni sababu ya viongozi wa tume hiyo kuteuliwa na Rais mbona viongozi wa mahakama wamekuwa wakiteuliwa na kiongozi huyo lakini hakuna malalamiko.

Kuhusu suala la wafanyakazi wanaopelekwa nje ya nchi kwa kutumia mawakala, Mhagama alisema Serikali ilipiga marufuku watu kupelekwa nje ya nchi kufanya kazi mwaka 2018 kutokana na ukiukwaji wa taratibu.

“Kuna kampuni hazikuwa na usajili na kwamba kama kuna mfanyakazi alipelekwa 2018 alienda isivyo halali” alisema.

Advertisement