Mtangazaji wa Clouds Gardner afariki, mastaa wamlilia
Muktasari:
Gardner maarufu kama Kapteni amefariki dunia akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Dar es Salaam. Mtangazaji maarufu wa kituo cha redio cha Clouds FM, Gardner G Habash amefariki dunia. Msemaji wa Kampuni ya Clouds Media Group, Emilian Mallya amethibitisha kifo cha mtangazaji huyo.
Gardner, mtangazaji wa kipindi cha Jahazi amefariki dunia akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) leo Aprili 20, 2024, saa 11 alfajiri.
“Ni kweli kwa taarifa za awali amefariki, lakini nitatoa taarifa zaidi baadaye,” amesema Mallya.
Wamlilia Gardner
Kupitia mitandao ya kijamii baadhi ya watu wakiwamo wasanii nyota nchini wametuma rambirambi kwa kifo cha Gardner.
Zamaradi Mketema, aliyewahi kuwa mfanyakazi mwenzake, kupitia mtandao wa Instagram ameandika:
“Aaah Gadna jamani! Inalillahi waina ilaihi rajiun! Mungu akupumzishe kwa amani kaka, Dah! Gadna, pumzika kwa amani kaka! Kazi ya Mungu haina makosa.”
Msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Peter Msechu kupitia Instagram amendika: “Daaaah aiseee pumzika Brother Gardner.”
Mwingizaji wa filamu, Steve Nyerere kupitia mtandao wa Instagram ameandika:
“Mstafuuuuu. Hapa duniani tunapita na barabara tunayopita ni wote tutapita hiyohiyo, bahati nzuri njia tunayopita kila mmoja ana muda wake wa kupita, lakini atapita tu. Maskini atapita, tajiri atapita chizi atapita, lakini tumepishana saa tu.”
Kupitia andiko lake, Steve amesema Mungu kaweka siri kubwa kwenye kifo ndiyo maana mpaka leo tumekuwa watu wa kusema Mungu nisaidie kifo chema.
“Kaka lala, tutaonana baadaye, ni ngumu kuamini, lakini kwa mapenzi ya Mungu kila jambo linawezekana,” amehitimisha andiko lake Steve.
Msanii Dulla Makabila kupitia mtandao wa Instagram ameandika kwa Kiingereza: “Pumzika kwa Amani kaka Gardner.”
Akaendelea kwa lugha ya Kiswahili alisema: “Mungu aitie nguvu familia, ndugu jamaa na mrafiki kwenye kipindi hiki kigumu.”
Kinjekitile Ngombale maarufu Kinje kupitia mtandao wa Instagram ameandika: “Rest in peace mdogo wangu. Juzi nimekuja kukuona nikakuambia nitakuja kukuona tena, daah! pumzika kwa amani mdogo wangu.”
Gardner alijipatia umaarufu kupitia kipindi cha Jahazi wakati huo akishirikiana na hayati Ephraim Kibonde, na Paul James maarufu PJ.
Kipindi hicho kilikuwa kikirushwa hewani kuanzia saa 10.00 jioni hadi saa 12.00 jioni.