Mtanzania ateuliwa katibu mkuu mpya wa EAC
Balozi Stephen Mbundi ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Picha na Mtandao
Muktasari:
- Mpaka anateuliwa leo kushika wadhifa huo, Mbundi ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania anayehusika na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Arusha. Balozi Stephen Mbundi ambaye ni Mtanzania, ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Mbundi ni Mtanzania wa pili kushika nafasi hiyo baada ya hayati Juma Mwapachu.
Mbundi aliyezaliwa mwaka 1968 Kinondoni, jijini Dar es Salaam na kupata elimu yake ya Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda na baadaye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ataiongoza taasisi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka huu 2026 hadi 2031.
Balozi Mbundi ametangazwa leo Jumamosi, Machi 7, 2026 katika Mkutano wa kawaida wa 25 wa wakuu wa nchi za EAC, uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Mkutano huo pamoja na mambo mengine, umewakutanisha viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo ya Afrika Mashariki kujadili pia masuala ya ushirikiano wa kikanda, maendeleo ya kiuchumi na mustakabali wa jumuiya hiyo.
Balozi Mbundi amekuwa mtumishi wa Serikali kwa kipindi cha miaka 28 katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, alikokuwa akishiriki kwa karibu vikao muhimu vya majadiliano na uamuzi kuhusu jumuiya kwa kipindi cha miaka 19.
Mpaka anateuliwa leo kushika wadhifa huo, Mbundi ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania anayehusika na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kuteuliwa kwa Balozi Mbundi kumetangazwa na mtangulizi wake, Veronica Nduva katika mkutano huo wa 25 wa wakuu wa nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki.
Baada ya kutangazwa, ameapishwa mbele ya wakuu hao wa nchi za EAC waliohudhuria mkutano.
Nduva amesema kukamilika kwa uteuzi huo sasa kunajenga uimara wa nchi waanzilishi ambazo ni Tanzania, Kenya na Uganda kuendelea kushikilia nafasi hiyo ili kusimamia malengo ya kuanzishwa kwake.
Mfumo mpya wa michango
Wakati huohuo, wakuu hao wa nchi wamepitisha mfumo mpya wa michango ya fedha kwa nchi wanachama ili kupunguza mgogoro wa kifedha unaoikabili taasisi hiyo.
Uamuzi huo umefikiwa kufuatia changamoto ya ucheleweshaji wa michango ya baadhi ya nchi wanachama na kusababisha jumuiya hiyo kukumbwa na uhaba wa fedha, hali inayoathiri utekelezaji wa baadhi ya shughuli mbalimbali za kikanda.
Akihutubia katika Mkutano huo, Mwenyekiti wa mkutano huo na Rais wa Kenya, William Ruto, amesema viongozi wa jumuiya wamekubaliana kubadili mfumo wa awali wa michango ili uwe wa haki zaidi kwa nchi zote wanachama.
Amesema chini ya mfumo huo mpya, michango ya nchi wanachama itagawanywa kwa uwiano wa asilimia 50 sawa kwa nchi zote, na asilimia 50 nyingine itazingatia ukubwa wa uchumi wa kila nchi unaopimwa kupitia pato la Taifa (GDP).
“Badala ya kila nchi kuchangia kiwango sawa, tumekubaliana kwamba asilimia 50 ya mchango itakuwa sawa kwa wote na asilimia nyingine 50 itategemea ukubwa wa uchumi wa nchi husika,” amesema Ruto.
Amesema mfumo huo mpya ni marekebisho ya pendekezo la awali lililotolewa na Baraza la Mawaziri la EAC ambalo limekaa jijini Arusha kwa siku tatu mfululizo.
Amesema awali ilipendekezwa kuwa michango igawanywe kwa uwiano wa asilimia 65 sawa kwa wote na asilimia 35 kulingana na uwezo wa kiuchumi wa nchi wanachama.
Mbali na marekebisho ya mfumo wa michango, wakuu wa nchi pia wamekubaliana kupunguza mzigo wa kifedha kwa kuondoa asilimia 50 ya madeni ya nyuma ya nchi wanachama, huku asilimia iliyosalia ikitakiwa kulipwa ndani ya miaka miwili.
Katika hatua nyingine ya kupunguza gharama za uendeshaji wa jumuiya, viongozi hao wamepitisha uamuzi wa kubadili mfumo wa malipo ya wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA).
Ruto amesema EALA ambayo hutumia zaidi ya asilimia 35 kwa mishahara yao, sasa italipwa na mabunge ya nchi zao badala ya bajeti ya EAC.
Kwa mujibu wa takwimu rasmi za jumuiya hiyo, hadi kufikia Januari 31, 2026, EAC ilikuwa inadai jumla ya dola za Marekani 89,372,865 kama michango ambayo haijawasilishwa na baadhi ya nchi wanachama.
Katika orodha ya nchi zenye madeni makubwa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inaongoza kwa deni la dola 27 milioni, ikifuatiwa na Burundi dola 22.7 milioni, Sudan Kusini dola 21.8 milioni na Somalia dola 10.5 milioni.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha hivi karibuni, Katibu Mkuu wa EAC, Veronica Nduva alisema hadi sasa ni nchi nne pekee ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda ndizo zilizokamilisha michango yake kwa wakati hadi mwaka wa fedha 2025/2026.
Alisema changamoto ya ucheleweshaji wa michango imeifanya jumuiya kuanza kutafakari mfumo endelevu zaidi wa ufadhili ambao utazingatia uwezo halisi wa kiuchumi wa nchi wanachama.
“Tumelazimika kuchukua hatua hii baada ya kutambua kuwa nchi wanachama haziko katika kiwango kimoja cha ukuaji wa uchumi au uwezo wa kukusanya mapato,” alisema Nduva.
Kwa mujibu wa taarifa za bajeti zilizowasilishwa katika kikao cha mtandao cha Bunge la EALA, jumuiya ilipitisha bajeti ya dola milioni 109.3 kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la EAC na Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki wa Kenya, Beatrice Askul Moe, alisema asilimia 62 ya bajeti hiyo sawa na dola 67.76 milioni inatarajiwa kutoka kwenye michango ya nchi wanachama, huku washirika wa maendeleo wakichangia asilimia 38 iliyobaki.