Mtoto abakwa akitokea kanisani Mufindi

Muktasari:

  • Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoani Iringa, ACP Sunday Songwe amesema kuwa tukio hilo limetokea Novemba 28, saa 11 jioni baada ya mtuhumiwa kumlaghai mtoto huyo kuwa kuna mtoto ndani ya nyumba yake ameanguka hivyo anahitaji msaada.

Mufindi. Jeshi la Polisi mkoani Iringa linamtafuta Yogi Mtavangu, Mkazi wa Mafinga wilayani Mufindi kwa tuhuma za kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 14, mkazi wa Mtaa wa Osterbay-Machinjioni, wakati akitokea kanisani kwenye ibada.

Tukio hilo limetokea wakati dunia ikiwa katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu Novemba 30, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoani Iringa, ACP Sunday Songwe amesema kuwa tukio hilo limetokea Novemba 28, saa 11 jioni baada ya mtuhumiwa kumlaghai mtoto huyo kuwa kuna mtoto ndani ameanguka hivyo anahitaji msaada.

“Alimdanganya kwamba kuna mtoto anahitaji msaada hivyo aende kumsaidia na alipoingia ndipo mtuhumiwa alifunga mlango na kumbaka,” amesema Songwe.

Akizungumza na Mwananchi leo, mtoto huyo amesema kuwa siku ya Jumapili wakati anarudi nyumbani akitokea kanisani alikutana na kijana mmoja njiani aliyemwita akisema kuna mtoto amezimia ndani kwake, hivyo aende kumuangalia kama atakuwa anamfahamu.

“Nilipoingia akafunga mlango na alinisukumiza kwenye kochi akaniambia nisipige kelele, anaweza hata kuniua ndipo akanibaka.

“Baada ya kunifanyia hivyo akafungua mlango akangalia nje kama kutakuwa kuna watu ndipo akaniambia niende kwani nje kuna watoto wanacheza na akanipatia Sh2, 000 akisema ninunue soda,” amefafanua mtoto huyo


Awali akisimulia tukio hilo, mjumbe wa Mtaa wa Osterbey wilayani hapa, Flora Luganga amesema alipigiwa simu akiambiwa kuwa kuna binti anatoka mtaani kwao kwamba amebakwa katika mtaa wa Jangwani na amekimbilia kanisani kwa ajili ya kuomba msaada.

“Baada ya kupigia simu hiyo niliondoka na kwenda eneo la tukio hadi kanisani ambapo mtoto huyo alikwenda kwa ajili ya kuomba msaada na kueleza kuwa amebakwa na kijana mmoja kutoka mtaa wa Jangwani,” ameeleza.

Mjumbe huyo asema kuwa baada ya kufika kanisani hapo walimchukua kisha kwenda kuomba nyumba ya jirani kwa ajili ya kuwangalia kama kweli anachosema kuwa maebakwa ni kweli au la.

“Baada ya kumkagua tuliubaini ni kweli mtoto huyo amefanyiwa ukatili huo na kuchukua hadi kituo cha polisi kwa ajili ya taratibu zingine zaidi,” amesema Luganga.

Kwa upande wake mama mzazi wa binti huyo, Eminata Mzena amesema hajafurahishwa na kitendo ambacho mtoto wake amefanyiwa bila Polisi kuchukua hatua zozote za kumkamata mtuhumiwa

“Sijatendelewa haki mimi kama mama ambaye nimebeba mimba miezi tisa viongozi wa serikali ya mtaa wamenisaidia lakini polisi hawajanisaidia kumkamata mtu ambaye amemfanyia ukatili mwanangu hivyo naomba serikali iweze kunisaida kuhusu jambo hili,” amesema Mzazi huyo.

Baba mzazi wa binti, Majuto Joseph amesema kuwa mke wake alifutilia hatua zote na alielekezwa juzi waende dawati ya jinsia kwa sababu wao ndio wafuatiliaji wa matukio hayo lakini hadi sasa hakuna msaada wowote ambao wameweza kusaidiwa. 

Naye Johnas Mnyagala ambaye ni fundi sofa na Mkazi wa Mtaa huo ameiomba Serikali kuingia kati suala hilo ili Mtuhumiwa aliyefanya kitendo hicho anakamtwa na mtoto huyo anapata haki yake.

Amesema umasikini isiwe chanzo cha watoto wao kubakiwa kutokana na ukosefu wa kipato kutokana na vitendo hivyo vimekuwa vikitokea na kuwaumiza wananchi wa hali ya chini.