Mtoto adaiwa kujinyonga Dodoma

Muktasari:
- Mtoto wa umri wa miaka 14 amekutwa amejinyonga kwenye mti ulio nje ya nyumba yao huku kukiwa hakuna taarifa za sababu za kujiua.
Dodoma. Mtoto mwenye umri wa miaka 14 anayefahamika kwa jina la Mpali Steven (14), amekutwa amefariki kwa madai ya kujinyonga kwenye mti uliopo nje ya nyumba yao katika Kijiji cha Mahomanyika, jijini Dodoma.
Tukio hilo limetokea leo Alhamisi Oktoba 5, 2023 huku sababu za kijana huyo kujinyonga zikiwa hazifahamiki.
Akizungumza na Mwananchi, Balozi wa Mtaa huo Msese Zakaria amesema walisikia kelele za kuomba msaada majira ya saa 12 asubuhi na walipofika eneo la tukio walikuta kijana huyo amejinyonga kwa kutumia kamba kwenye mti uliopo nje ya nyumba yao.
Zakaria amesema baada ya kukuta tukio hilo walianza kutoa taarifa kwa viongozi wa ngazi za juu za Kijiji ambapo walitoa taarifa polisi.
"Polisi wamekuja hapa wakachukua mwili wa marehemu na kuondoka nao pia wakawachukua wazazi wote wawili wa marehemu, baadhi ya majirani na mimi Balozi ambapo wametuchukua maelezo na kutuachia, pia wameruhusu tuzike kesho," amesema Zakaria.
Amesema mpaka polisi wanauchukua mwili na kufanyia uchunguzi hawajapata maelezo yoyote yanayoonyesha sababu za kijana huyo kujinyonga.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji hicho Ernest Kutona amesema walipata taarifa za tukio hilo asubuhi na mapema kupitia kwa Balozi wa Mtaa lilipotokea tukio hilo na kwamba waliwajulisha polisi ambao walifika na kuchukua mwili.
Amesema kutokana na hali waliyoikuta hakuna hata mtu mmoja aliyeweza kumkagua marehemu huyo kwenye mifuko ya suruali aliyokuwa ameivaa ili kujua kama ameacha ujumbe wowote.
Amesema kwa taarifa alizozipata kijana huyo alikuwa hasomi.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Dodoma, Martin Otieno amesema hana taarifa za tukio hilo na kusema kuwa atafuatilia ili ajue ukweli wake.