Mtoto adaiwa kuua mwenzake kwa risasi

Mtoto adaiwa kuua mwenzake kwa risasi

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi mkoa wa Ilala linamshikilia Juma Shamata kwa kushindwa kuhifadhi eneo salama bastola yake, hali iliyosababisha mtoto wake wa miaka 17 kuitumia kwa kumpiga risasi mtoto mwenzie Ikhissan Abdilahi (10) na kumsababishia kifo.

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi mkoa wa Ilala linamshikilia Juma Shamata kwa kushindwa kuhifadhi eneo salama bastola yake, hali iliyosababisha mtoto wake wa miaka 17 kuitumia kwa kumpiga risasi mtoto mwenzie Ikhissan Abdilahi (10) na kumsababishia kifo.

Jeshi hilo pia linamshikilia mtoto huyo wa kidato cha tatu kwa tuhuma za mauaji.

Tukio hilo lilitokea Aprili 2 katika mtaa wa Viwege kata ya Pugu nyumbani kwa Shamata ambako Ikhissan alikwenda kucheza.

Kwa mujibu wa mashuhuda, baada ya Ikhissan kuingia kwenye nyumba hiyo walisikia kishindo na punde mtoto aliyefanya tukio hilo alitoka akiwa amembeba na kumrejesha nyumbani kwao akieleza kuwa amepigwa na shoti ya umeme.

Shangazi wa marehemu aitwaye Aisha Hussen alisema; “Nilikuwa nimekaa kwenye kibaraza hapa nje, Ikhissan alikuwa anaendesha baiskeli, alipofika pale (kwenye nyumba aliyopigwa risasi) akaingia ndani, baada ya muda mfupi tukasikia mlio mkali, lakini hakuna aliyehisi kwamba inaweza kuwa risasi.

“Ghafla akatokea mtoto wa nyumba ile akiwa amembeba Ikhissan na kumleta hapa nje ya geti akamuacha akisema kwamba amepigwa na shoti ya umeme, nilimkimbilia nikamchukua kumuingiza ndani kwa ajili ya huduma ya kwanza maana alikuwa akivuja damu,” alisema Aisha.

Baada ya kumchunguza kwa dakika kadhaa waligundua kuwa alikuwa na tundu kifuani ambalo lilitokeza upande wa pili ndipo walipomuwahisha hospitali ambako waliarifiwa kuwa ameshafariki dunia.

Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Kipolisi Ilala, Moses Fundi alisema yupo mtoto aliyekuwa anacheza na mwenzake kisha kumjeruhi na risasi iliyopelekea kupoteza maisha.

Kamanda Fundi alisema jeshi hilo linamshikilia mwanafunzi huyo na baba yake kwaajili ya mahojiano ili kujua ukweli wa tukio hilo.

Kamanda huyo alisema uchunguzi wa awali wa polisi umebaini kuwa kulikuwa na uzembe katika uhifadhi wa silaha hiyo, jambo lililosababisha mtoto kuifikia.

Alisema kuwa silaha haiwezi kuhifadhiwa sehemu kama juu ya kabati, kama mtu anamiliki silaha utaratibu wa kuhifadhi unafahamika, ikiwamo kuifungia kwenye sanduku la chuma.

“Tumegundua silaha inamilikiwa kihalali, lakini inawezekana kuna uzembe katika utunzaji wa silaha hiyo, kama mtoto anaweza kuichukua ina maana hata mwizi angekuja angeweza kuichukua,” alisema kamanda Fundi.