Mtoto akamatwa akidaiwa kumlawiti mwenzake Njombe

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga

Muktasari:

  • Mtuhumiwa (12) aliacha shule akiwa darasa la sita naamekuwa akimfanyia hivi vitendo mtoto wa miaka 10 kwa muda mrefu.

Njombe. Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe linamshikilia mtoto wa umri wa miaka (12) kwa tuhuma za kumlawiti mwanafunzi wa darasa la nne (10) katika shule moja iliyopo Makambako mkoani Njombe.

Hayo yamebainishwa leo Aprili 13, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe Mahamoud Banga zungumza na waandishi wa habari mkoani hapa.

Amesema tukio hilo lilitokea Aprili 4, 2024 Mtaa wa Jeshini mjini Makambako.

Amesema mwanafunzi huyo alikuwa akilawitiwa kwa ahadi ya kupewa fedha na mtuhumiwa huyo ambaye aliacha shule akiwa darasa la sita.

"Mtuhumiwa huyu anaonekana aliacha shule akiwa darasa la sita lakini amekuwa akimfanyia hivi vitendo kwa muda mrefu kwa ahadi ya kumpatia fedha," amesema Banga.

Amesema kwa muda wote huo mwanafunzi huyo hakusema kwa wazazi lakini tabia yake ilianza kubadilika baada ya kuwa anatokwa na haja kubwa na baada ya mama yake kumwadhibu, ndipo alisema kuwa anafanyiwa vitendo hivyo.

Ongezeko la matukio ya ulawiti hapa nchini Tanzania ni tatizo linalozidi kuongezeka, hususan kutokana na kuibuka kwa matikio yanayohusisha watoto, hali hii inaleta wasiwasi kwa jamii na kuathiri maendeleo ya kijamii na ustawi wa watoto.

Hii ni aina ya unyanyasaji wa kijinsia ambao unahusisha kutumia nguvu au ulaghai, na ni matukio yanayokandamiza haki za binadamu na kusababisha madhara makubwa kisaikolojia, kimwili na kijamii kwa wahusika, hususan watoto.

Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya mji wa Makambako, Masinde Masinde amesema matukio ya ulawiti kwa sasa yamekuwa mengi hivyo wazazi wanatakiwa kuwa karibu na watoto ili kuwalinda na vitendo hivyo.

"Niwaombe wazazi watimize jukumu lao la malezi ili kuwalinda katika suala zima la ukatili hasa huu uliokithiri wa ubakaji na ulawiti," amesema Masinde.

Mjumbe wa nyumba 10 katika eneo hilo, Charles Mkane ameiomba Serikali kuwachukulia hatua za kisheria watu wote ambao wanatajwa kuhusika na vitendo vya ulawiti kwa kuwa vimekuwa vikikithiri siku hadi siku.

"Watoto wanaofanya vitendo vya ulawiti wakamatwe ikiwezekana kuwepo na msako wa polisi ili kukomesha vitendo hivyo vya ubakaji na ulawiti," amesema Mkane.

Mama mzazi wa mtoto anayedaiwa kulawitiwa amesema alibaini changamoto hiyo baada ya kuona kila anapofua nguo za mtoto wake zinakuwa na uchafu wa haja kubwa.

"Nimekutwa na changamoto ya ukatili kwa mwanangu na amefanyiwa na mtoto mwenzake kwa kulawitiwa kwa muda mrefu," amesema.