Prime
Mtoto alivyosababisha kifo cha kaka yake katika mchezo wa fimbo wa Wasukuma
Picha ikiwaonesha vijana wa kiume wa kabila la Wasukuma wakiwa katika mchezo wa kupigana fimbo kama sehemu ya mila na desturi yao. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Julai 6, 2025, katika kijiji cha Mtenga, wilaya ya Nkasi, mkoani Rukwa, Jackson Kayoka alishindwa kujikinga na mashambulizi ya fimbo kutoka kwa ndugu yake, na kusababisha kifo chake bila kukusudia.
Sumbawanga. Kwa wanaume wa kabila la Wasukuma, mchezo wa kupigana fimbo ni mila na desturi yao, lakini siku zote hazifanani, kwani mchezo huo ndio ulisababisha kifo cha ndugu wakati akipigana fimbo.
Julai 6, 2025, katika kijiji cha Mtenga, Wilaya ya Nkasi, mkoani Rukwa, Jackson Kayoka alishindwa kujikinga na mashambulizi ya fimbo kutoka kwa ndugu yake mwenye umri wa miaka 14, na kusababisha kifo chake bila kukusudia.
Kutokana na namna mauaji hayo yalivyofanyika na ripoti ya ustawi wa jamii kuhusu jinsi ya kushughulika na wakosaji watoto, Jaji Thadeo Mwenempazi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga alimwachia huru mtoto huyo kwa masharti.
Jaji Mwenempazi alitoa hukumu hiyo Aprili 27, 2026, baada ya mtoto huyo kusomewa shtaka la kuua bila kukusudia na maelezo ya kosa, kisha akakiri kuwa maelezo hayo yalikuwa ya kweli na sahihi, hivyo mahakama ikamtia hatiani.
“Ripoti imewasilishwa mahakamani ikionesha kuwa mtoto huyo alizaliwa mwaka 2009 katika Kijiji cha Mtakumbuka, Kata ya Fimbo, wilaya ya Tanganyika, na baadaye kuhamia Kijiji cha Mtenga ambako amekuwa akiishi.
“Amekuwa akiishi na wazazi wake tangu kuzaliwa. Kulingana na ripoti hiyo, tabia yake iliathiriwa na mambo ya vijana, mazoea ya kitamaduni, ushawishi wa marika, na ukosefu wa ujuzi juu ya malezi na usimamizi sahihi kutoka kwa jamaa zake,” alisema jaji.
Alisema Ofisa Ustawi wa Jamii ameialika mahakama kuzingatia Kanuni ya 49(1) ya Kanuni za Uendeshaji Mashauri ya Mtoto, na akataja kifungu cha 116(1), (2) na (3) cha Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 kuhusu hukumu kwa mtoto.
“Pia imependekezwa, kwa kuzingatia kumweka mkosaji mtoto chini ya amri ya uangalizi chini ya Kanuni ya 52(1) ya Sheria ya Mtoto (Taratibu za Mahakama ya Watoto) za mwaka 2016, G.N. Na. 182 ya 2016, na kuwasilishwa mpango uliopendekezwa endapo mahakama itazingatia kutoa amri hiyo ya uangalizi,” alieleza Jaji Mwenempazi.
“Nimezingatia shtaka, ukweli unaojumuisha kosa, jinsi kosa lilivyofanyika, mawasilisho ya Mwanasheria wa Serikali na wakili wa utetezi, ripoti ya Ofisa Ustawi wa Jamii, pamoja na sheria inayosimamia ushughulikiaji wa wakosaji watoto.
“Ninaamua kwamba mshtakiwa anahukumiwa kuachiliwa kwa masharti chini ya Kanuni ya 50(1), (2) na (3)(a), na kuwekwa chini ya usimamizi wa mlezi wake kwa ushirikiano na wazazi na jamaa wengine,” alisema, na kuongeza:
“Mzazi na mtoto wataripoti katika Ofisi ya Ustawi wa Jamii ya Wilaya kwa ajili ya ushauri nasaha kila Ijumaa ya mwisho wa mwezi, kwa wakati na mahali palipowekwa, kwa muda wa mwaka mmoja, kama ilivyopendekezwa.”
Tukio lilivyotokea
Kulingana na maelezo ya kosa hilo, Julai 6, 2025, mtoto huyo pamoja na ndugu yake walikuwa wakicheza mchezo maarufu wa kabila la Wasukuma wa kuchapana fimbo, ambao huchezwa na wanaume.
Hata hivyo, kwa bahati mbaya, Jackson aliteleza na kushindwa kujilinda kutokana na pigo la fimbo la mshtakiwa, na kusababisha jeraha kubwa kichwani lililosababisha majeraha makubwa na hatimaye kifo dakika chache baadaye.
Dk Stella Hokororo alifanya uchunguzi wa mwili wa marehemu na kubaini majeraha juu ya kichwa pamoja na jeraha nyuma ya kichwa,hivyo akaeleza kuwa chanzo cha kifo ni kutokwa na damu ndani ya kichwa.
Siku ya hukumu ilivyokuwa
Upande wa mashtaka, uliowakilishwa na Wakili wa Serikali, Mwanaisha Liwawa, ulieleza kuwa mshtakiwa ni mkosaji wa mara ya kwanza, hivyo kuiomba mahakama impe adhabu inayostahili kwa mujibu wa sheria za nchi.
Kwa upande wake, wakili wa utetezi, Tumpe Mwaijumba, alisema kwa kuwa mshtakiwa ni mkosaji wa mara ya kwanza, aliiomba mahakama impe adhabu ndogo kwa sababu kifo hicho kilitokea kwa bahati mbaya na hakikukusudiwa.
Wakili huyo alijenga hoja pia kuwa mshtakiwa ni mtoto mwenye umri wa miaka 14, hivyo akapendekeza aachiliwe huru kwa masharti kwa kuwa bado ni mwanafunzi, na kuachiliwa kwake kutamuwezesha kuendelea na masomo.
Kabla ya kutoa hukumu hiyo, jaji alifafanua kuwa ni utaratibu wa kisheria chini ya Sheria ya Mtoto kwamba pale mshtakiwa anapokuwa mtoto, ni lazima Ofisa Ustawi wa Jamii afanye uchunguzi na kuwasilisha ripoti yake mahakamani.