Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mtoto aliyetekwa apatikana hai msituni, baba adaiwa kuhusika

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Jumatatu Juni 15,2026.

Muktasari:

  • Razaki anayesoma elimu ya awali katika Shule ya Msingi Mwakimome, aliripotiwa kutekwa Juni Mosi, 2026 katika Kata ya Katumba Songwe, Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya.

Mbeya. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kupitia kikosi maalumu cha kupambana na uhalifu, limefanikiwa kumpata mtoto Razaki Mwakatundu (5) aliyekuwa ameripotiwa kutekwa akiwa hai.

Mtoto huyo amepatikana akiwa ametelekezwa katika Msitu wa Hifadhi ya Kitulo, mpakani mwa mikoa ya Mbeya na Njombe.

Razaki anayesoma elimu ya awali katika Shule ya Msingi Mwakimome, aliripotiwa kutekwa Juni Mosi, 2026 katika Kata ya Katumba Songwe, Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya.

Kwa mujibu wa taarifa za awali, mtoto huyo alichukuliwa alipokuwa akicheza na wenzake nje ya nyumba yao.

Hata hivyo taarifa zilizopatikana zinadai kuwa baba mzazi wa mtoto huyo anadaiwa kumchukua na kuondoka naye kusikojulikana.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu, Juni 15, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amethibitisha kupatikana kwa mtoto huyo akiwa hai baada ya msako uliofanywa na Jeshi la Polisi.

“Mtoto huyo aliripotiwa kutekwa na mtu anayesadikiwa kuwa baba yake mzazi akiwa anacheza na wenzake, kisha kuondolewa na kupelekwa kusikojulikana,” amedai Kamanda Kuzaga.

Amesema uchunguzi wa awali umebaini tukio hilo linahusishwa na mgogoro wa kifamilia, ambapo mtuhumiwa alidaiwa kutaka kurejeshewa mahari ya Sh500,000 baada ya mama wa mtoto kukataa kuendeleza uhusiano na mwanaume huyo.

“Kitendo hicho kilitokana na kutoridhishwa na uamuzi wa mama wa mtoto jambo lililomfanya mtuhumiwa kuchukua hatua hiyo isiyo ya kisheria,” amedai kamanda huyo.

Amesema baada ya taarifa hiyo kuripotiwa, Jeshi la Polisi lilianza msako na limefanikiwa kumpata mtoto huyo akiwa ametelekezwa katika ya Msitu wa Hifadhi ya Kitulo akiwa hai.

Amesema juhudi za kumsaka mtuhumiwa zinaendelea huku kukiwa na taarifa kwamba ametoweka baada ya kubaini kuwa polisi wanamtafuta.

“Tutahakikisha mtuhumiwa anapatikana na kufikishwa mahakamani ili hatua za kisheria zichukuliwe,” amesema.

Aidha, Kamanda Kuzaga ametoa wito kwa wazazi na walezi kuepuka kujichukulia sheria mkononi katika migogoro ya kifamilia, akisisitiza kuwa vitendo hivyo vinahatarisha usalama wa watoto na kuleta taharuki kwa jamii.

Katika tukio jingine, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Idd Hussein, mkazi wa Kimara, Dar es Salaam kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi yenye uzito wa kilo 30.

Kamanda Kuzaga amesema mtuhumiwa alikamatwa Juni 14, 2026 saa 1:30 usiku katika kizuizi cha Polisi cha Mafiga kilichopo Kata ya Kasumulu, Tarafa ya Unyakyusa, Wilaya ya Kyela.

Amesema bangi hiyo ilikuwa imefungashwa katika vifurushi 13 na kuhifadhiwa ndani ya begi kubwa la plastiki pamoja na begi la mgongoni.

“Uchunguzi wa awali umebaini mtuhumiwa ni msafirishaji na muuzaji wa dawa za kulevya na atafikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa,” amesema.