Mtoto asimulia mwenzake alivyofariki kwa kufukiwa na kifusi
Mtoto aliyefariki kwa kufukiwa na kifusi, Eda Jonathan (10) enzi za uhai wake
Muktasari:
- Mtoto huyo, Eda Jonathan (10) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tatu Shule ya Ilemela English Medium iliyopo wilayani Ilemela mkoani humo alifariki kwa kufukiwa na kifusi kwenye shimo Jumamosi Agosti 24, 2024. Tayari mwili wake umesafirishwa kwenda mkoani Dodoma kwenye familia yake kwa ajili ya mazishi.
Mwanza. Mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Ilemela English Medium iliyopo Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, Eda Jonathan (10) amefariki dunia kwa kufukiwa na kifusi wakati akitafuta fedha Sh1,000 kwenye shimo linalochimbwa moramu.
Eda alifariki Jumamosi Agosti 24, 2024, katika shimo linalotumika kuchimba moramu lililoko katika Shule ya Gederi, Kata ya Mecco wilayani Ilemela, huku mtoto mwingine aliyekuwa naye akijeruhiwa paja la mguu wa kulia.
Shuhuda wa tukio hilo ambaye ni mtoto wa miaka saba (jina linahifadhiwa) ameieleza Mwananchi kuwa siku hiyo baada ya kuagizwa dukani kwenda kununua mkaa, walipita eneo la shule hiyo huku wakicheza, jambo lililosababisha wapoteze Sh1,000 waliyopewa kununua mkaa huo.
Akionekana mwenye hofu, mtoto huyo amesema baada ya kupoteza fedha hiyo, Eda na Junior waliamua kuingia ndani ya shimo hilo kuitafuta ndipo gema la shimo hilo lilipotitia na kuwafukia, jambo lililomfanya ajawe hofu na kukimbia kutoa taarifa nyumbani.
“Baada ya kuona Eda na kaka Junior wamefukiwa, nilikimbia kwenda kumwambia mama, akawaita watu wengine wakaja kuwasaidia. Lakini niliona tu baadaye wametolewa,” anasema mtoto huyo.
Huku akibubujikwa machozi, mama mkubwa wa marehemu, Patricia Ludovick amesema tukio hilo lilitokea akiwa ameenda Nyakato Sokoni kununua mahitaji ya familia ndipo alipopigiwa simu na jirani yake kuwa Eda amefariki kwa kufukiwa na kifusi.
“Ilikuwa Jumamosi saa 7 mchana, nimetoka nyumbani nimeenda National Nyakato Sokoni, nikapigiwa simu kwamba Eda amedondokewa na kifusi, nikachukua pikipiki hadi pale, kweli nikakuta Eda amefariki,” amesema Patricia.
Kwa mujibu wa Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Gederi Kata ya Mecco wilayani humo, Frank Ndekeja tayari uongozi wa mtaa huo umetoa maelekezo kwa uongozi wa shule hiyo kufukia shimo hilo zikiwa zimepita siku nne tangu kutokea tukio hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amethibitisha kutokea tukio hilo huku akimtaja aliyefariki kuwa ni Eda Jonathan (10) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tatu, Shule ya Ilemela English Medium, na aliyejeruhiwa kuwa ni Junior Kilinga (6) ambaye anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Bugando.
“Tukio hili lilitokea Agosti 24, 2024, saa 7 mchana huko Gederi Mecco Wilaya ya Ilemela, huyu Eda (marehemu) akiwa na watoto wenzake wawili ambao ni Simon Kilinga (7) na mwenzake mwenye umri wa miaka sita waliangukiwa na kifusi na kusababisha kifo cha Eda,” amesema Mutafungwa.
Kamanda huyo amesema watoto hao walikumbwa na mkasa huo baada ya kuagizwa mkaa na mama aitwaye Zawadi James (18).
“Walivyopita pale kulikuwa na shimo kubwa lililochimbwa na wanafunzi wa shule hiyo wakichukua Moramu. Sasa wakati wanacheza eneo hilo wakapoteza Sh1,000 waliyokuwa wametumwa kununua mkaa basi watoto wawili ambao ni Eda na Junior wakaingia kuitafuta ndipo kifusi kikawaangukia na kuwafunika,” amesema kamanda huyo.
Kamanda Mutafungwa amezitaka taasisi na mitaa ambayo ina mashimo ya aina hiyo kuyafukia ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza kwa watu wakiwemo watoto.