Mtoto ateketea kwa moto askari wakiendesha operesheni kuondoa wavamizi

Mtoto ateketea kwa moto askari wakiendesha operesheni kuondoa wavamizi

Muktasari:

  • Mtoto Nyanzore Ng'wandu (4) amefariki dunia kwa kuteketea kwa moto wakati wa operesheni ya kuwaondoa wananchi waliovamia eneo tengefu ndani ya Hifadhi ya jamii Isawimo inayoundwa na vijiji 11 vya Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora.

Mwanza. Mtoto Nyanzore Ng'wandu (4) amefariki dunia kwa kuteketea kwa moto wakati wa operesheni ya kuwaondoa wananchi waliovamia eneo tengefu ndani ya Hifadhi ya jamii Isawimo inayoundwa na vijiji 11 vya Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu jana Ijumaa Juni 18, 2021 mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Abel Busalama amethibitisha kifo cha mtoto huyo kilichotokea wakati wa operesheni iliyofanyika Juni 16, 2021.

Mtoto aliyetekea kwa moto ni mjukuu wa mzee Ng'ombeikungire Ng'wandu, mkazi wa kijiji cha Kombe wilayani Kaliua.

"Serikali imesikitishwa na kifo cha mtoto huyo na vyombo vya dola vimeanza uchunguzi wa kuhusu tukio hilo. Mimi binafsi nimefika eneo hilo nikiongozana na kamati ya usalama ya wilaya."

"Kuna maswali na hoja nyingi kuhusu kifo cha mtoto yule, kwanza wana familia wanasema aliteketea baada ya kuanguka mlangoni katika jitihada za kujiokoa. Lakini eneo mwili upokutwa ni karibia hatua mbili kutoka mlangoni," amesema.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya, kuna hisia kuwa kifo cha mtoto huyo ni tukio la kutengenezwa kwa nia ya kukwamisha operesheni ya kuwaondoa waliovamia eneo la hifadhi na kuendesha shughuli za kibinadamu ikiwemo makazi, kilimo, uvuvi na ufugaji.

"Siwezi kusema kwa uhakika ni nani ametengeneza tukio hilo lakini mazingira yanatia shaka na ndio maana vyombo vinafanya uchunguzi wa kina," amesema mkuu huyo wa wilaya

Akizungumzia tukio hilo, diwani wa Usinge, Titus Kavura amelaani kitendo cha askari Mamlaka ya Wanyamapori na Jeshi la Polisi walioshiriki operesheni hiyo kutumia nguvu na mabavu badala ya busara kiasi cha kuteketeza nyumba bila kutoa fursa kwa wananchi kujiokoa na kuokoa mali.

"Walichokuwa wanafanya askari wale ni kufika na kutia moto nyumba bila kujali ndani kuna watu wala mgonjwa,  hii ndio maana wazazi walitimua mbio kujiokoa na kumsahau mtoto aliyekuwa amelala ndani," amesema diwani Kavura.