Mtoto wa Askofu Sepeku aibua mapya mahakamani

Muktasari:
- Bernado alifungua kesi ya madai Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, akipinga kunyang’anywa zawadi ya kiwanja alichopewa baba yake na kanisa hilo.
Dar es Salaam. Mtoto wa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, marehemu John Sepeku, Bernardo Sepeku (63) amedai kuwa walimuandikia barua, aliyekuwa askofu wa tatu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Basil Sambano, alipoingia tu madarakani mwaka 1992.
Bernardo amedai kuwa lengo la kumwandikia barua askofu Sambano lilikuwa ni kumpa taarifa na kumjulisha mchakato ulivyofanyika hadi baba yao kupewa zawadi ya kiwanja na nyumba na kanisa hilo.
Amedai kuwa walimuandikia barua hiyo kutokana na barua aliyokuwa amewaandikia kabla ya kuwa askofu, wakati huo akiwa padri, ambapo katika barua yake alieleza kuwa kuna watu ambao hawatapata hati za umiliki kutokana na jinsi walivyopewa hayo maeneo.
Bernardo ametoa maelezo hayo leo Mei 8, 2025 Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, wakati akitoa ushahidi wake katika kesi ya ardhi iliyoifunguliwa yeye, dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Askofu Jackson Sostenes wa kanisa hilo pamoja na Kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd.
Bernado, alifungua kesi hiyo ya ardhi namba 378/2023, akipinga kunyang’anywa zawadi ya kiwanja alichopewa baba yake mwaka 1978 na kanisa hilo.
Sepeku alipewa zawadi na kanisa hilo ambayo ni nyumba iliyopo Buguruni na kiwanja chenye ukubwa wa ekari 20 kilichopo Buza, wilayani Temeke, kama zawadi kwa kutambua mchango wake katika kanisa hilo.
Katika kesi hiyo, anadai alipwe Sh3.72bilioni ambayo ni fidia ya hasara ya kifedha iliyopatikana kutokana na uvamizi wa mali ya ardhi katika kiwanja hicho.
Pia anaiomba alipwe fidia ya Sh493.65 milioni ambayo ingepatikana baada ya kukomaa na mavuno ya mazao yaliyokuwepo kwenye shamba hilo.
Hata hivyo, wakati kesi hiyo ikiendelea na usikilizwaji, mdaiwa wa tatu katika shauri hilo, kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd, hajawahi kufika mahakamani hapo tangu kesi hiyo ilipofunguliwa licha ya kupokea wito wa kuitwa mahakamani.
Akitoa ushahidi wake mbele ya Jaji Arafa Msafiri, Bernardo amedai Juni 28, 1996, kaka yake na Bernardo, Julius Sepeku alimuandikia barua Askofu Basil Mwambano kumueleza mtitiriko mzima wa mchakato mzima ulivyompa baba yao zawadi ya kiwanja kilichopo Buza na nyumba iliyopo Buguruni.
"Vile vile tulikuwa tunamkumbusha kuwa askofu Sambamo ndio alikuwa mjumbe namba 11 kwenye kikao cha Sinodi kilichopitisha yale maazimino ya baba kupewa zawadi ya ekari 20 za shamba kule Buza pamoja na nyumba moja iliyopo Buguruni" amedai Bernardo.
Akiongozwa kutoa ushahidi wake na wakili Deogratias Butawantemi akishirikiana na Gwamaka Sekela, amedai mwaka 1978 na 1980 kulifanyika mkutano mkuu wa Sinodi ambapo pamoja mambo mengine ulipendekeza baba apewe zawadi, baada ya kustaafu utumishi wake.
Bernardo ameeleza hayo wakati alipoitwa Mahakama hapo kukamilisha kutoa ushahidi wake, baada ya ushahidi wake kwanza kutoa Machi 28, 2025 na kesi hiyo kuahirishwa hadi leo, kutokana na muda kuisha.
Alidai kuwa mkutano huo ulikuwa ni mahususi kwa ajili ya mapendekezo ya kutoa zawadi kwa askofu Sepetu.
Amedai kuwa, Julius ambaye amefariki dunia mwaka 2009 , alishawahi kushika nyadhifa mbalimbali Serikali, kama Msaidizi wa raisi mwaka 1962, Katibu Mkuu Msaidizi Ikulu kuanzia Mwaka 1970 hadi 1990 na Katibu Mkuu wa Wizara mbalimbali kama Habari, Mawasiliano, Uchukuzi, Maliasili, Afya na Viwanda na Biashara kuanzia mwaka 1970 hadi 1990.
Pia, Julius alishawahi kuwa Katibu wa tume ya Jaji Francis Nyalali na tume ya Jaji Warioba.
" Matokeo ya barua tuliyomwandikia askofu Sambano ilitusaidia kwa sababu askofu Sambano alituambia tushunghulikie wenyewe ili tuweze kupata hati ya umiliki ya kiwanja na kutokana na maelezo hayo kama familia tuliaanza mchakato wa kupima eneo hilo na kuweka alama za mipaka na mchakato huu, ulimalizika awamu ya nne ya askofu Mokiwa" amedai.
Hata hivyo pamoja na kupima eneo lao, bado hawajapata hati ya umiliki la shamba hilo.
Alipoulizwa na wakili wa wadaiwa, Dennis Malamba, iwapo mirathi imefungwa, alidai kuwa haijafungwa.
Alipoulizwa iwapo Halmashauri ya kudumu ya Sinodi ndio wenye mamlaka ya kutoa zawadi? Alijibu kuwa ndio wenye mamlaka.
Baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake, aliuliza maswali kadhaa ya dodoso na wakili wa wadaiwa, wakili Dennis Malamba.
Baada ya kumaliza kuhojiwa, Jaji Msafiri aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 14, 2025 kwa ajili ya kuendele na usikilizwaji.