Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Padri Mwamazi atoa ushahidi kwa njia ya video

Muktasari:

  • Bernado, mtoto wa hayati Askofu John Sepeku amefungua kesi ya ardhi namba 378/2023 akipinga kunyang’anywa zawadi ya kiwanja alichopewa baba yake mwaka 1978.

Dar es Salaam. Aliyekuwa Padri wa Kanisa Anglikana, Dayosisi ya Dar es Salaam, John Mwamazi (91) ametoa ushahidi kwa njia ya video akiwa nyumbani kwake Mbezi Luis, kutokana na matatizo ya kiafya.

Alitoa ushahidi jana Desemba 17, 2024 katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi kwenye kesi ya ardhi iliyofunguliwa Bernardo Sepeku dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Askofu Jackson Sostenes wa kanisa hilo na Kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd.

Bernado, ambaye ni mtoto wa hayati Askofu John Sepeku, alifungua kesi ya ardhi namba 378/2023, akipinga kunyang’anywa zawadi ya kiwanja alichopewa baba yake mwaka 1978 na kanisa hilo.

Askofu Sepeku alipewa na kanisa hilo nyumba iliyopo Buguruni na kiwanja chenye ukubwa wa ekari 20 kilichopo Buza, wilayani Temeke, kama zawadi kwa kutambua mchango wake katika kanisa hilo, akiwa askofu mkuu wa kwanza kanisa hilo.

Bernardo anadai alipwe Sh3.72 bilioni ambayo ni fidia ya hasara ya kifedha iliyopatikana kutokana na uvamizi wa mali na ardhi katika kiwanja hicho.

Pia anaomba alipwe fidia ya Sh493.65 milioni ambayo ingepatikana baada ya kukomaa mavuno ya mazao yaliyokuwamo shambani.

Licha ya usikilizwaji wa kesi kuendelea, mdaiwa wa tatu katika shauri hilo, kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd, hajawahi kufika mahakamani tangu kesi ilipofunguliwa licha ya kupokea wito wa kuitwa mahakamani.

Padre Mwamazi ametumia saa moja na nusu kutoa ushahidi akiwa amekaa kwenye kiti maalumu kutokana na kukabiliwa na tatizo la uti wa mgongo, ambalo limesababisha ashindwe kufika mahakamani.

Mahakama ilielezwa shahidi hawezi kusimama wala kutembea.

Kutokana na hali hiyo, mtaalamu wa Tehama wa mahakama alifunga televisheni kubwa iliyokaa katikati ya meza na nyingine ndogo upande wa wakili aliyemuongoza kutoa ushahidi ambazo ziliunganishwa kumwezesha kutoa ushahidi.

Akiongozwa kutoa ushahidi na wakili Deogratias Butawantemi, mbele ya Jaji Arafa Msafiri, shahidi amedai kikao cha Desemba 8, 1978 kilichoketi katika ofisi ya askofu iliyopo Kipalapala eneo la Upanga, kwa kauli moja kilipitisha azimio la kumpatia nyumba ya kuishi na eneo, aliyekuwa Askofu Mkuu wa kwanza wa Kanisa la Anglikana Tanzania, hayati John Sepeku.

Amedai kikao hicho kilikuwa na ajenda mbili, moja ilisimamiwa na mwenyekiti wa kikao Sepuku na ya pili ilikuwa kujadili zawadi anayopewa askofu huyo.

Ameeleza wajumbe walimuondoa Sepeku katika kikao ili wajadiliane wenyewe.

Padri Mwamazi ambaye ni shahidi wa tano wa upande wa mdai, ameeleza kipindi hicho alikuwa mjumbe wa halmashauri ya kudumu ya Sinodi. Alidai mkutano huo ulikuwa mahususi kwa ajili ya mapendekezo ya kutoa zawadi kwa askofu huyo aliyekuwa mkuu wa kwanza tangu kuanzishwa kwa kanisa hilo mwaka 1970.

“Katika mkutano huo nilikuwa mjumbe namba saba, kikao kilipitisha Askofu Sepeku apewe zawadi ya ekari 20 za shamba kwa kuwa alikuwa anaelekea kustaafu.

"Nimefanya kazi katika Dayosisi ya Dar es Salaam kwa miaka 43, hivyo nalifahamu vizuri eneo hilo la shamba lenye ukubwa wa hekta 410 lililopo Buza," amedai.

Ameeleza alikuwa shemasi mwaka 1960 na Oktoba 1963 aliteuliwa kuwa padri Zanzibar. Mwaka 1964 alihamishiwa Dar es Salaam na kuendelea na wadhifa huo hadi alipostaafu 2007.

Shahidi aliomba maelezo yake yapokewe na mahakama yawe sehemu ya kielelezo katika kesi hiyo, ombi ambalo halikupingwa na upande wa wadaiwa.

Baada ya kumaliza kutoa ushahidi, wakili wa mdaiwa wa kwanza na wa pili katika kesi hiyo, Dennis Malamba alimuuliza maswali ya dodoso, baadhi ya maswali yakiwa yafuatayo:


Wakili: Shahidi katika aya ya tano ya maelezo yako uliyoyatoa mahakamani hapa, umesema wakati Dayosisi ya Dar es Salaam ilipoanzishwa mwaka 1965, Askofu Sepuku alikuwa wa kwanza na wewe ulikuwa nani?

Shahidi: Padri

Wakili: Aya ya nane ya maelezo yako umeeleza kikao mlichokaa Desemba 8, 1978 kiliongozwa na nani?

Shahidi: Kiliongozwa na John Sepeku.

Wakili: Hicho kikao alichoongoza baba Askofu Sepeku, huoni kwamba alijipatia hii zawadi yeye mwenyewe?

Shahidi: Hapana, hakujipatia.

Wakili: Hiki kikao kiliitwa na nani?

Shahidi: Katibu wa Sinodi.

Wakili: Sinodi gani?

Shahidi: Sinodi ya Dayosisi ya Dar es Salaam.

Wakili: Shahidi wakati unatoa ushahidi wako na kuwasilisha maelezo yako, Dayosisi ya Dar es Salaam ni sehemu ya hii kesi?

Shahidi: Hapana

Wakili: Mzee Mwamazi, shamba la Buza linamilikiwa na nani hadi keshokutwa?

Shahidi: Ni mali ya Dayosisi ya Dar es Salaam.

Wakili: Dayosisi ya Dar es Salaam, ilipataje hili shamba?

Shahidi: Lilinunuliwa na Askofu Charles Allan Smythies, ambazo hekta 410 zipo Buza na hekta 53 zipo Buguruni Kichwele.

Shahidi amedai eneo hilo lilikuwa maalumu kwa ajili ya kuwahifadhi watumwa wanaotoka Zanzibar ambao hawana ndugu. Ameeleza walipofika Tanzania, walikuwa wanapelekwa eneo hilo kwa ajili ya kuishi na kulima mazao ya chakula.

Wakili: Huyo Askafu Charles alikuwa anafanya kazi katika kanisa lipi?

Shahidi: Kanisa la Anglikana la Uingereza. Baada ya kugawanyika kwa kanisa la Tanzania, tulitengeneza jimbo letu na ndiyo lilichukua mali zote na mwaka 1970 tukawa na bodi ya wadhamini.

Wakili: Dayosisi ya Dar es Salaam ilishawahi kuwa na bodi ya wadhamini?

Shahidi: Ina Bodi ya Jimbo la Dar es Salaam.

Wakili: Utakubaliana na mimi kwamba usipokuwa na wadhamini huwezi kumiliki mali?

Shahidi: Mali zipo Bodi ya Jimbo.

Wakili: Shahidi, wewe umekuwepo muda mrefu katika kanisa je? Shamba la Buza hati yake inasoma nani?

Shahidi: Dayosisi ya Dar es Salaam.

Wakili: Siyo Registered Trustee of The Anglican Church of Tanzania?

Shahidi: Hao siyo walipa kodi.

Wakili: Kwa hiyo malipo yenu yote ya ardhi yanalipwa kwa Dayosisi ya Dar es Salaam au serikalini?

Shahidi: Serikalini.

Baada ya wakili Malamba kumaliza kumhoji shahidi juu ya ushahidi wa maandishi alioutoa mahakamani, Jaji Msafiri alisema maelezo ya shahidi yamepokewa na mahakama hiyo na kuwa kielelezo katika kesi hiyo ambayo imepangwa kuendelea leo Desemba 18, 2024.