Mtoto wa miaka 15 aliyeolewa ajeruhiwa kwa kipigo na mumewe
Muktasari:
- Mtoto mdogo wa miaka 15 ambaye tayari ameolewa amejeruhiwa baada ya kupigwa na mumewe, Namendea Lesiria kwa tuhuma ya kumwaga dawa ya mifugo.
Longido. Mtoto mdogo wa miaka 15 ambaye tayari ameolewa amejeruhiwa baada ya kupigwa na mumewe, Namendea Lesiria kwa tuhuma ya kumwaga dawa ya mifugo.
Mtoto huyo makazi wa Kijiji cha Gelailumbwa, Kata ya Gelailumbwa, Wilayani Longido Mkoa wa Arusha amejeruhiwa maeneo mbalimbali ya mwili na kumwachia makovu ikiwemo usoni mwake.
Mtoto huyo amebainika baada ya leo Alhamisi Septemba 22, 2022 kufikishwa kituo cha afya Longido kwa ajili ya matibabu na maofisa wa ustawi wa jamii.
Ofisa Ustawi wa Jamii wilayani humo, Atunagile Chisunga amesema tayari mtuhumiwa Lesiria na ambaye anadaiwa kushiriana na rafiki yake, wamefikishwa kituo cha Polisi Longido na kesho Ijumaa wanatarajia kufikishwa mahakamani.
"Huu ni ukatili kabisa, kwanza ameolewa akiwa na umri mdogo, wamempiga wakiwa wamemfunga kamba na kumtundika kwenye miti na kusababisha majeraha makubwa," amesema Chisunga
Naye Mratibu wa dawati la jinsia katika Shirika la Wanahabari la Kusaidia Jamii za Pembezoni (MAIPAC), Debora Makando ameiomba Serikali kuchukuwa hatua kali kwa vijana ambao bado wananyanyasa watoto
"Huu ni ukatili mkubwa, kwanza huyu binti ni mtoto ameolewa lakini pia kupigwa hivi haikubaliki," amesema
Katika baadhi ya jamii za pembezoni bado watoto wamekuwa wakiolewa na kufanyiwa ukatili ikiwepo kupigwa na kukeketwa.