Mtoto wa Mwinyi azikwa

Muktasari:

  • Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi leo Agosti 31, 2022 amejumuika na viongozi wa kitaifa, Chama cha Mapinduzi (CCM) na mamia ya wananchi katika maziko ya kaka yake Hassan Ali Mwinyi (66) yaliofanyika Mangapwani Mkoa Kaskazini Unguja.

Zanzibar. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi leo Agosti 31, 2022 amejumuika na viongozi wa kitaifa, Chama cha Mapinduzi (CCM) na mamia ya wananchi katika maziko ya kaka yake Hassan Ali Mwinyi (66) yaliofanyika Mangapwani Mkoa Kaskazini Unguja.

Hassan alifariki dunia Agosti 30, 2022 usiku katika Hospitali ya Mnazi Mmoja hapa alikokuwa amelazwa kwa muda mrefu.

Maandalizi ya maziko ya marehemu Hassan yalifanyika nyumbani kwake  Chukwani Mkoa Mjini Magharibi, ambapo wananchi, ndugu na jamaa pamoja  na majirani  walipata fursa ya kumswalia na  baadaye mwili wake kusafirishwa hadi Mangapwani, ambako aliswaliwa tena na kuzikwa kwenye shamba  la familia.

Akitoa nasaha baada ya kukamilika kwa hafla ya dua na swala, mjumbe wa Maulamaa Mkoa Kaskazini Unguja, Sheikh Khamis Abdulhamid aliwataka waislamu kumuombea marehemu huyo, huku akiitaka familia kuwa na moyo wa subra.

Naye, Balozi wa Tanzania nchini Saud Arabia, Mwadini akiwasilisha salamu kwa Rais mstaafu wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Zanzibar Dk Mwinyi pamoja na wanafamilia, kwa niaba ya mabalozi hao, alimuombea pumziko jema kwa Mwenyezi Mungu marehemu.

Aidha, akitoa salamu kwa niaba ya Kikosi Kazi Tanzania, Sheikh Mkuu wa  Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Alhad Mussa alitoa pole kwa familia na kuwataka kuwa na subira kwa kipindi hiki cha majonzi.

Akitoa shukrani kwa niaba ya familia ya marehemu, ndugu wa marehemu huyo, Abdalla Ali Mwinyi aliwashukuru wananchi wote walioungana na familia katika msiba huo mzito wa ndugu yao.

Hassan Ali Mwinyi akiwa mtoto wa pili wa familia ya Rais mstaafu wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, ameacha mjane na watoto saba.

Katika kipindi cha uhai wake aliwahi kuwa mtumishi wa Umma na miongoni mwa nyadhifa alizoshika ni pamoja na kuwa Meneja wa Shirika la Meli Zanzibar.

Pamoja na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa viongozi wengine walioshiriki maziko hayo ni, Rais mstaafu wa Zanzibar, Abeid Amani Karume, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla na Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania, Mizengo Pinda.