Mtoto wa Sauli aliza watu akiweka shada kwenye kaburi la baba yake
Muktasari:
- Katika ajali hiyo, Sauli alikuwa na mtoto wake Adrich (miaka mitatu) kwenye gari ambaye alinusurika na kubakiwa na majeraha ya kichwani
Chunya. Adrich Mwalabila (3), mtoto wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Mabasi ya Sauli, Solomon Mwalabila maarufu kwa jina la Sauli (46), amewatoa machozi mamia ya watu baada ya kuitwa kwa ajili ya kuweka shada la maua kwenye kaburi la baba yake.
Adrich alinusurika kifo katika ajali hiyo iliyochukua uhai wa baba yake Agosti 4, 2024 eneo la Mlandizi mkoani Pwani baada ya gari alilokuwa akiliendesha Sauli kugongwa na lori lililokuwa limebeba mchanga.
Katika maziko hayo yaliyofanyika leo Jumatano Agosti 7, 2024 Kijiji cha Godima, wake wa marehemu wakiongozwa na Evaline Bahati ndio walitangulia kuweka shada la maua kwenye kaburi wakafuatiwa na mama mzazi wa marehemu, Hilda Mwasenga ambaye hata hivyo alishindwa kunyanyuka kutoka kwenye kiti kutokana na huzuni.
Adrich akiwa anaweka shada hilo la maua juu ya kaburi la baba yake, kelele za vilio kutoka kwa waombolezaji iliongezeka huku kila mmoja akijisemesha kivyake.
Adrich, ambaye aliumia kichwani katika ajali hiyo, alifika eneo la kaburi na kushikishwa shada na mmoja wa watu wa karibu na familia, kisha akaweka juu ya kaburi huku akionekana imara.
Maziko hayo ya Sauli yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwamo Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mmbarack Batenga, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga, Mbunge wa Lupa, Masache Kasaka na viongozi wengine wa kisiasa.