Mtoto, waganga kortini wakidaiwa kumuua ‘muuguzi’ KCMC
Muktasari:
- Waganga wawili wa Jadi na mwanamke Wendy Mrema (41) ambaye ni mtoto wa marehemu, wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kumuua kwa makusudi mama yake mzazi ambaye ni muuguzi mstaafu wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Patricia Ibreck (66)
Moshi. Waganga wawili wa jadi na mwanamke Wendy Mrema (41) ambaye ni mtoto wa marehemu, wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kumuua kwa makusudi muuguzi mstaafu wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Patricia Ibreck (66) ambaye ni mama mzazi wa Wendy.
Wendy ambaye ni mshitakiwa wa pili katika kesi hiyo, ameunganishwa na Omary Rang’ambo (32) ambaye ni mshitakiwa wa kwanza mkazi wa jijini na Dar Es Salaam na Waziri Ally (37) ambaye ni mshitakiwa wa tatu na wote ni waganga wa jadi.
Patricia alitoweka nyumbani kwake eneo hilo la Rau nje ya mji wa Moshi tangu Februari 2021 hadi mwili wake ulipofukuliwa Januari 9, 2022 na mabaki yake kupatikana huku ndani ya kaburi kukikutwa pia panga lililokuwa na nyewele.
Washitakiwa hao walisomewa mashitaka ya mauaji ya kukusudia leo Januari 26, 2022 mbele ya Hakimu Mkazi Moshi, Rehema Olambo na hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Akiwasomea mashitaka hayo, wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS) kanda ya Moshi, Agatha Pima alidai Januari 9, 2022 katika wilaya ya Moshi, washitakiwa walimuua kwa makusudi Patricia kinyume cha sheria.