Mtumbwi uliobeba wanafunzi wapinduka, wawili waokolewa

Muktasari:

Wanafunzi wanne kati ya sita wa Shule ya Msingi Kagera Manispaa ya Kigoma Ujiji wanahofiwa kusombwa na maji ya Mto Luiche baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kupinduka na kuzama.

Kigoma. Wanafunzi wanne wa Shule ya Msingi Kagera Manispaa ya Kigoma Ujiji, wanahofiwa kuzama majini baada ya mtumbwi walilokuwa wamepanda kupinduka na kuzama ndani ya mto Luiche.

Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Salum Kali amesema tukio hilo limetokea Saa 1:30 asubuhi leo Ijumaa Februari 24, 2023 wakati wanafunzi hao wakiwa na wenzao wawili wakivuka kutoka mtaa wa Mgumile kwenda shuleni ya msingi iliyoko mtaa wa Kagera.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu akiwa eneo la tukio, Kali amesema juhudi za uokoaji zinaendelea na tayari wanafunzi wawili na nahodha wa mtumbwi wameokolewa.

“Wanafunzi wanne wanahofiwa kuzama ndani ya maji ya mto Luiche inayomwaga maji yake ndani ya Ziwa Tanganyika baada ya mtumbwi wao kupinduka kutokana na kuzudiwa kasi ya maji,”amesema Kali

Amesema kwa kawaida, wakazi wa Kata ya Kagera wakiwemo wa mtaa wa Mgumile walikotoka wanafunzi hao hutumia mitumbwi huvuka mto Luiche kila siku asubuhi na jioni kwenda mitaa mingine kwa shughuli za kiuchumi na kijamii ikiwemo shuleni.

“Kwa bahati mbaya leo mtumbwi walilopanda wanafunzi limepigwa na mawimbi ya maji ya mto ambao umajaa kutokana na mvua zilizonyesha jana,” amesema Kali

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu akiwa eneo la tukio, Diwani wa Kata ya Kagera, Gregory Ebelezo amewataja wanafunzi wanaohofiwa kusombwa na maji kuwa ni Ashura Ramadhani na Tatu Hasan wanaosoma darasa la kwanza, Zabibu Masoud wa darasa la pili na Ramadhani Matatizo anayesoma darasa la tano.

Wakazi wa Kata ya Kagera iliyoko takriban umbali ya Kilometa 12 kutoka katikati ya mji wa Kigoma wanaokadiriwwa kuwa zaidi ya 9, 000 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 wamekuwa wakiiomba Serikali kuwajengea daraja kuwanusuru na adha ya kuvuka mto kwa mitumbwi isiyo salama.

Licha ya adha ya kutumia mitumbwi inayoongozwa kwa kutumia miti, wakazi wa kata hiyo pia hulazimika kutumia kati ya Sh400 hadi Sh1, 000 kwa ajili ya nauli ya mitumbwi.

Mto Luiche ambao maji yake huenda kwa kasi, hasa unapojaa pia una wanyama wakali akiwamo mamba na viboko.