Mufti atangaza mwezi kuandama, Idd el Fitri kesho

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ametoa ujumbe akihimiza umoja, haki na ukarimu.

Dar es Salaam. Mufti wa Tanzania, Abubakar Zuberi leo Jumanne Aprili 9, 2024 ametangaza kuandama kwa mwezi na hivyo sikukuu ya Idd el Fitri itakuwa kesho Jumatano Aprili 10.

Akizungumza na vyombo vya habari, Sheikh Mkuu Zuberi amesema mwezi umeandama maeneo mbalimbali ikiwamo Zanzibar.

Kuandama kwa mwezi kunahitimisha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

“Ndugu Waislamu leo Aprili 9, 2024 nimepokea taarifa ya mwezi kuandama kutoka Kenya na pia kutoka hapa nyumbani. Zanzibar katika eneo la Pemba, kwa mujibu wa ofisi ya Mufti wa Zanzibar imetujulisha kuwa mwezi umethibiti na wao wameuthibitisha, hivyo basi mimi kama Mufti wa Tanzania, nauthibitisha mwezi huo na taarifa, hivyo kesho Aprili 10, 2024 itakuwa Idd el Fitri. Niwatakie Idd njema,” amesema.

“Na kwa utaratibu wetu, Idd itaswaliwa hapa makao makuu (ya Bakwata, Kinondoni) na jioni kutakuwa na baraza la Idd katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNICC),” amesema.

Bodi ya wakurugenzi na menejimenti ya Mwananchi Communications Ltd inawatakia heri Waislamu na Watanzania wote katika Sikukuu ya Idd el Fitri.
Mufti wa Zanzibar kupitia taarifa kwa umma aliyoitoa leo amebainisha kuwapo kwa sikukuu kesho.

“Ofisi ya Mufti Mkuu Zanzibar inawaarifu Waislamu wote wa Zanzibar kuwa leo mwezi umeandama, hivyo kesho siku ya Jumatano Aprili 10, 2024 ni sawa na mwezi 1 Shawwal (mfunguo Mosi),” imesema sehemu ya taarifa hiyo.


Salamu za Mbowe

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ametoa ujumbe wa sikukuu hiyo kupitia kurasa zake za mitandao ya kijimii akisema:

“Eid Mubarak. Katika sherehe hii njema ya Eid ul-Fitr, natoa salamu zangu za dhati na kuwatakia yote yaliyo mema kwa Waislamu wote duniani. Nawaombea siku hii iwe imejaa amani, furaha, na baraka kwenu na kwa wapendwa wenu.”

“Tunaposherehekea mwisho wa Ramadhani, tukumbuke masomo ya subira, huruma, haki, na shukrani ambayo mwezi huu mtukufu umetufundisha. Tuendeleze roho ya umoja, haki na ukarimu tunapoadhimisha siku hii maalumu.”

“Mungu awabariki na akubali sala zenu na saumu, na Eid hii ikatuweke karibu zaidi na yeye na kwa kila mmoja. Tujitahidi kueneza upendo, wema, haki na uelewano katika jamii zetu, na matendo yenu yaakisi kiini cha kweli cha Uislamu. Salaam Aleykum!”