Muhongo aagiza Rea iwatimue makandarasi wazembe Julai

“Napenda kutoa agizo kupitia Bunge lako kuwa ikifika Julai Mosi mkandarasi ambaye atakuwa hajaanza kazi, Rea lazima wamtoe waweke mwingine.”Profesa Muhongo.

 

Muktasari:

  • Profesa Muhongo alisema hayo bungeni jana akijibu hoja mbalimbali za wabunge zilizotolewa wakati wakichangia Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2014/2015.

Dodoma. Waziri wa Nishati na Madini, Profesa  Sospeter Muhongo ameiagiza Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) kuwafutia mikataba makandarasi wote ambao watakuwa hawajaanza kazi ifikapo Julai Mosi, mwaka huu.

Profesa Muhongo alisema hayo bungeni jana akijibu hoja mbalimbali za wabunge zilizotolewa wakati wakichangia Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2014/2015.

“Napenda kutoa agizo kupitia Bunge lako kuwa ikifika Julai Mosi mkandarasi ambaye atakuwa hajaanza kazi, Rea lazima wamtoe waweke mwingine,” alisema Profesa Muhongo.

Aidha, aliwataka mameneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kuhakikisha kuwa wateja wanaoomba kufungiwa umeme katika vijiji vilivyopo pembezoni mwa miji hawatozwi gharama za kuunganisha umeme za mijini.

“Vijiji vilivyoko pembezoni mwa miji ni wale watu wana mazizi ya ng’ombe, wana makaburi ya wazee wao, naomba wale wapewe umeme kwa gharama za wanavijiji,” alisema. Alisema gharama za kuwaunganishia wateja hao katika awamu ya pili ya Rea ni Sh27,000 na Sh5,000 kwa ajili ya ada ya fomu ya maombi.

“Hakuna rushwa, hakuna hongo na kampuni ambayo

italetwa wizarani kuwa wafanyakazi wake wameomba rushwa itanyang’anywa kazi na tumeshakubaliana hivyo,” alisema.

Wachimbaji wadogo kupewa ruzuku

Kuhusu wachimbaji wadogo wa madini, Profesa Muhongo, alisema Serikali katika bajeti ya mwaka huu, itawapa wachimbaji wadogo wa madini ruzuku ya Dola za Marekani 50,000 (Sh80 milioni) ambazo hawatatakiwa kuzirejesha.

“Nendeni mkawaambie wachimbaji wadogo kuwa wakati wa neema ni sasa... Tunawapatia bure tunataka waboreshe uchimbaji wao,” alisema.

Mwakyembe kicheko

Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amewataka wabunge kuwapongeza mawaziri wa fedha kwa sababu fedha zote walizoomba kwa ajili ya utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), kwenye sekta  ya reli zimetolewa.

“Nilitarajia katika mkutano huu Waziri wa Fedha na manaibu wake wapongezwe kwelikweli kwa kufanikisha miradi yote ya BRN ambayo kwa kweli imekwenda kwa asilimia 95,” alisema na kuongeza:

“Wamefanya hivyo si kwa kuipendelea wizara ila kwa sababu ya kutambua kuwa sekta ya uchukuzi ni muhimu katika kuleta mabadiliko ya uchumi nchini.”

Dk Mwakyembe alisema Shirika la Reli lilipobinafsishwa halikuleta mafanikio kama mashirika mengine na ndiyo maana Serikali iliamua kulichukua.