Mume adaiwa kumuua mkewe, kujeruhi kichanga kwa kisu

Muktasari:

  • Fausta Tesha (26), mkazi wa Mero wilaya ya  Moshi, Mkoani Kilimanjaro ameuawa kwa kukatwa na kisu sehemu mbalimbali za mwili wake na kisha mwanaye wa wiki mbili kujeruhiwa kwa kisu na kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya kanda ya Kaskazini (KCMC).

Moshi. Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro linamshikilia mwanaume mmoja, mkazi wa Mero, wilaya ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro kwa madai ya kumuua mkewe na kumjeruhi mtoto mchanga kwa kile kinachodaiwa ni wivu wa mapenzi.

Mwanamke huyo ambaye anatambulika kwa jina la Fausta Tesha (26) aliuawa kwa kukatwa na kisu  sehemu za tumboni, kifuani na  ubavuni pamoja na kichanga chake usiku wa kumkia jana, Februari 23, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Polisi, mtoto huo mchanga wa wiki mbili amalezwa katika hospitali ya KCMC kwa ajili ya matibabu baada ya kuchomwa kisu tumboni na kusababisha utumbo kutoka nje.

Akizungumza na Mwananchi digital jana Februari 23, Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Simoni Maigwa amesema wanamshikilia mwanaume huyo kutokana na mauaji ya mke wake.

"Mwanaume huyu amemuua mke wake na kumjeruhi mtoto wa wiki mbili kwa wivu wa mapenzi, huyu mwanaume alienda kwenye machimbo huyu mwanamke akawa amepata ujauzito, sasa ikaonekana kuna mgogoro wa familia juu ya huyu mtoto," amesema.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kisare Makori amelaani tukio hilo na kutoa rai kwa wananchi kuacha tabia ya kuchukua sheria mkononi na kusema wanaofanya vitendo kama hivyo watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

"Serikali tunakemea vikali matukio kama haya na sio ustaarabu na kama kwenye familia kuna utofauti kuna vyombo vya sheria, hakuna sheria inayoruhusu mtu kumuua mwenzake kwasababu ya tofauti zao, kama kunakutofautiana basi vyombo vya sheria vipo na sio kuuana,” amesema.