Mume adaiwa kumuua mkewe kwa kumnyonga kisa kuchelewa kurudi nyumbani
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga
Muktasari:
- Taarifa zinaeleza kuwa mume na mke wote walikuwa watumiaji wa kilevi na siku hiyo walikuwa wanagombana huku wamelewa.
Njombe. Jeshi la polisi mkoani hapa linamshikilia Robert Chagavali (33) mkazi wa kijiji cha Kichiwa kwa tuhuma za mauaji ya mke wake, Nuru Mkula (32) chanzo kikitajwa ni kuchelewa kurudi nyumbani.
Hayo yamesemwa leo Machi 27, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga alipokuwa akizungumza na Mwananchi Digital mkoani hapa.
Amesema Machi 22,2024 saa nne asubuhi kulikuwa na ugomvi kati ya marehemu na mumewe chanzo kikidaiwa kuwa marehemu alitoka kwenye mashamba ambayo alikuwa anavuna ulanzi na kwenda kutafuta dawa, lakini alichelewa kurudi nyumbani.
Amesema Machi 23, 2024 kulitokea kutoelewana tena na kuanza kugombana, lakini baadaye ikaripotiwa tukio kuwa mwanamke huyo amefariki.
"Kwa hiyo Jeshi la Polisi tulifika eneo la tukio kwa ajili ya kukagua lakini tuliona kama kuna dalili na alama za miguu mingi kama kulikuwa na ugomvi kati ya hawa wawili" amesema Banga.
Amesema baada ya mwili wa marehemu kufikishwa kituo cha afya Makambako na kufanyiwa uchunguzi na daktari ilionekana shingo ya marehemu ilikuwa imenyongwa.
Kamanda Banka amesema inaonekana wazi kuwa aliyefanya tukio hilo ni mume wake ambaye jeshi hilo linamshikilia katika Kituo cha Polisi Makambako, na taratibu nyingine zinaendelea za kimashtaka dhidi ya mtuhumiwa huyo.
Amesema mtuhumiwa huyo anavyoonekana ni mtumiaji wa pombe za kienyeji na inaonekana kuwa siku ya tukio alitumia kilevi, ingawa hawakumpima na shughuli zake ni kugema ulanzi na kuuza.
"Wanasema wanaogema mara nyingi wanapata kinywaji kabla ya kwenda kwa wateja " amesema Banga.
Amewataka wananchi mkoani Njombe kupunguza unywaji wa pombe ya ulanzi kwa kuwa kiafya siyo nzuri na inaweza kukusababishia kufanya vitendo vya kikatili.
Mtendaji wa kijiji cha Mji Mwema, Maneno Mguta amesema marehemu na mume wake wote walikuwa watumiaji wa pombe ya ulanzi na siku ya tukio walikuwa wamelewa.
"Mama alikuwa anatumia hicho kinywaji na hata baba pia, marehemu h ameacha mtoto mdogo wa umri wa kama mwaka mmoja hivi" amesema Mguta.
Baadhi ya wananchi Njombe akiwemo Merygoreth Richard amelaani tukio hilo la kikatili na kuiomba Serikali kuendelea kutoa elimu itakayosaidia kupunguza vitendo vya kikatili mkoani humo.
"Kwa kweli vitendo hivi vimekithiri sana tunaomba elimu iendelee kutolewa kama mtu huwezi kuishi naye ni bora tu mkaachana, kuliko kufanya huu ukatili" amesema Richard.