Amuua mkewe kwa kumkata mapanga kisa wivu wa mapenzi
Muktasari:
- Mwanamme mmoja anayefahamika kwa jina la Golani Nh'umbu (35) anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Simiyu kwa tuhuma za kumkata na panga mkewe sehemu mbali mbali za mwili na kumsababishia kifo.
Maswa. Mwanamme mmoja anayefahamika kwa jina la Golani Nh'umbu (35) anashikiliwa na Jeshi la Polisi wilayani hapa kwa tuhuma za kumkata na panga mkewe sehemu mbali mbali za mwili na kumsababishia kifo.
Taarifa ya mauaji hayo imetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Blasius Chatanda amemtaja marehemu kuwa ni Pili Masonga (28) akisema tukio hilo limetokea Oktoba 17, 2021 katika kijiji cha Hinduki kata ya Malampaka wilayani hapa.
Anasema kutokana na kelele alizokuwa akipiga marehemu wananchi walijitokeza kwa lengo la kumsaidia ndipo walipo fanikiwa kumkamata mume wa marehemu akiwa ameshika panga kisha kumfikisha polisi.
Katika hatua nyingine, RPC Chatanda amesema mwanafunzi wa darasa la kwanza Japhet Milima miaka 13 amejeruhiwa na mnyama aina chui alipokuwa anachunga ng'ombe.
Amesema tukio hilo limetokea katika kijiji cha Mwabulimbu wilayani Maswa mkoani hapa ambapo watu wengine wawili walijeruhiwa wakati wakimuokoa mtoto huyo na kufanikiwa kumuua chui aliyekuwa amewavamia.