Mume wa miaka 102, mke miaka 90 wafunga ndoa

Muktasari:
Mzee wa Miaka (102) Masasila Kibuta Mkazi wa Kijiji cha Nyamazugo Wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza amefunga pingu za maisha na mke Chem Mayala (90) Kwa madai siku akitoka duniani akaonane na Mungu baada ya kutimiza agano la ndoa takatifu.
Sengerema. Kikongwe Masasila Kibuta (102) na mke wake Chem Mayala, wakazi wa Kijiji cha Nyamazugo Wilaya ya Sengerema wameingia kwenye historia ya wenza wenye umri mkubwa kufunga pingu za maisha baada ya kufunga katika Kanisa Katoriki Kigango cha Nyamazungo Parokia ya Ngomamtiba Wilaya ya Sengerema.
Ingekuwa katika mchezo wa Soka, usemi sahihi ambao ungefaa kuelezea kitendo cha wana ndoa hawa ingekuwa ule wa "haujaisha hadi uishe au mchezo ni dakika 90"
Ndoa ya vikongwe hao ambayo ni gumzo ndani na nje ya Wilaya ya Sengerema baada ya taarifa zao kusambaa imefungwa Juni 17, 2023 mbele Padre Julian Mondula wa Parokia ya Ngomamtimba.
Katika mafundisho yake wakati wa hafla hiyo ya kihistoria, Padre Jualian Mundula amewataka waumini wengine, hasa vijana ambao bado wanaishi kinyumba bila kufunga ndoa kuiga mfano wa wazee hao.
"Nawapongeza wana ndoa wetu wapya kwa uamuzi wa kijasiri wa kuamua kuhalalisha uhusiano wao kwa kufunga ndoa baada ya kuishi miaka mingi kama mume na mke," amesema Padre Mundula
Amewaasa wawili hao wapya kuendelea kuishi kwa upendo, uaminifu na uvumilivu katika raha na shida kwani huo ndio msingi na njia ya kuishi kwa amani na kudumu katika mahusiano.
Akizungumza baada ya kufunga ndoa, mzee Kibuta amesema uamuzi wao wa kufunga pingu za maisha umelenga kurekebisha mahusiano yao na Mungu ili hata wakifariki wakakutane naye huko Mbinguni
Amesema Chem Mayala ni mke wake wa pili baada ya mke wake wa kwanza kufariki dunia na wameishi miaka mingi nakufanikiwa kupata watoto 12, lakini hawakuwahi kufunga ndoa.
"Sasa hata tukifariki tutaenda kuonana na Mungu kwa sababu tayari tumetimiza agano kwa kufunga ndoa takatifu," amesema Mzee Kibuta akiwa na uso wenye bashasha
Shuhuda wa ndoa hiyo Mwalimu Japhet Makori wa Shule ya Sekondari Nyampulukano aliyewahi pia kufundisha katika shule ya Sekondari Nyamazugo amewapongeza wazee hao kwa kutimiza agano ya ndoa takatifu huku akiwaomba vijana kuiga mfano huo.
"Kwa kipindi chote nilichoishi na kufanya kazi Kijiji cha Nyamazugo, familia ya Mzee Kibuta ni miongoni mwa familia bora za kutolewa mfano. Licha ya umri wao mkubwa, wazee hawa wanaishi kwa upendo utafikiri ni watu waliooana juzi. Kwa kweli lipo la kujifunza kutoka kwao," amesema Mwalimu Makori