Muswada wa tume ya mipango wapita, sasa kuwa na waziri wake

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Muktasari:

  • Bunge limeupitisha muswada wa sheria ya tume ya mipango wa mwaka 2023, ambao sasa unatoa mwanya kwa tume hiyo kuwa na waziri wake atakayeiongoza.

Dododma. Bunge limepitisha Muswada wa Sheria ya Tume ya Mipango wa mwaka 2023 huku ikiondolewa Wizara ya Fedha na Mipango na kupelekwa kwa Ofisi ya Rais.

Muswada huo umewasilishwa na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene bungeni leo Alhamisi Juni 8, 2023.

Pamoja na mambo mengine, tume hiyo itakuwa na jukumu la kubuni, kupanga, kuratibu na kusimamia mipango ya maendeleo ili kuwa na mfumo jumuishi wa ufuatiliaji na tathimini ya utekelzaji wa vipaumbele vya maendeleo ya Taifa.

Majukumu mengine ni kuratibu na kupanga pamoja mipango ya kisekta, hususani zenye majukumu yanayoendana na kuwa na mfumo wa kisheria na chombo mahususi cha kusimamia uandaaji, utekelezaji wa mipango ya maendeleo utafiti na kuishauri Serikali kuhusu vipaumbele vya maendeleo ya Taifa.

Simbachawene alisema sheria imeweka masharti kuhusu uanzishwaji wa Tume ya Mipango, muundo, mamlaka na majukumu ya Tume ya Mipango.

“Tume ya Mipango itaongozwa na Rais kama Mwenyekiti na wajumbe wengine sitawatakaoteuliwa na Rais akiwemo waziri mwenye dhamana na masuala ya mipango ya maendeleo na waziri mwenye dhamana ya masuala ya fedha,” amesema Simbachawene.

Pia amesema sheria imebainisha nafasi ya Katibu Mtendaji wa Tume na naibu makatibu watendaji, lengo la muundo huo ni kuhakikisha tume inakuwa na uwezo wa kuratibu na kusimamia masuala yote ya mipango ya maendeleo ambayo ni kusimamia masuala ya ufuatiliaji na tathmini.

Simbachawene amesema ili kuiwezesha Tume kutekeleza majukumu haya kwa ufanisi, muswada wa sheria umeipa mamlaka ya kutoa miongozo, maelekezo na nyaraka mbalimbali za utekelezaji.

Amesema katibu mtendaji na naibu makatibu watendaji watateuliwa na Rais kupitia mchakato wa ushindani.

Na watumishi wengine watapatikana kwa utaratibu wa ushindani kwa kuzingatia vigezo vya weledi na uzoefu.

“Lengo ni kuhakikisha kuwa tume inapata watendaji nawatumishi wenye ujuzi, weledi na waliobobea katika masuala ya mipango ya uchumi na maendeleo kwa ujumla.”

 “Kama ilivyo kwa taasisi nyingine za umma zinazoendeshwa kwa bajeti ya Serikali, hesabu za tume zitakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali,” amefafanua waziri huyo.

Amesema muswada unatoa mamlaka ya waziri kutengeneza kanuni na kubainisha makosa na adhabu na tume imepewa mamlaka ya kuitisha taarifa yoyote kutoka kwa mtu au taasisi yoyote kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake.

Wabunge washauri

Kwa upande wa Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mashimba Ndaki amesema Kamati inashauri Serikali kutoa elimu kwa Wizara na taasisi zote za umma kuhusu mamlaka ya Tume katika kuandaa, kusimamia na kutoa miongozo ya mipango ya maendeleo.

“Hii itasaidia kufungamanisha Mipango inayoandaliwa na taasisi hizo na ile inayoandaliwa na Tume ili kuwianisha mipango ya kisekta katika mamlaka hizo na mipango ya Tume.”

“Aidha, elimu kwa umma itawezesha wadau wote kushiriki katika kuiwezesha Tume kwa kuipatia taarifa zitakazowezesha uandaaji na ufuatiliaji wa mipango ya maendeleo,” amesema Ndaki.

Mbunge wa Kawe (CCM), Joseph Gwajima amesema hofu yake ipo katika ulinzi wa mipango hiyo na kuhoji watafanyaje ili mipango inayopangwa itekelezwe.

“Chaguzi zinapoanza zinaandaliwa ilani za uchaguzi, ni muhimu ilani ya chama chochote cha siasa ilingane na mpango wa Taifa wa muda mrefu maana ilani ndio mkataba kati ya wananchi wanasiasa na chama hicho kikichukua madaraka huo ndio unakuwa mpango unaotekelezwa miaka mitano,” amesema.

Amesema ni muhimu ilani za uchaguzi za vyama zikakaguliwa na Tume ya Taifa ya Mipango kusudi chama kikiingia madarakani kiweze kutekeleza mpango husika.

Gwajima aliongeza kuwa, anaiona Tanzania mpya inakuja baada ya kuundwa kwa Tume ya Mipango iwapo mipango iliyowekwa itatekelezwa.

Mbunge wa Busanda (CCM), Tumaini Magesa amesema kuundwa kwa tume hiyo kutawezesha kupata mambo yaliyofanyika kwenye mipango ya maendeleo iliyopita.

“Muswada huu ulivyokuja katika kamati hawa watu walikuwa waende mtaani kukusanya mapato, kamati ilisema wazi wasilekeze kwenda kukusanya fedha tutapoteza mwelekeo wetu wa kutaka ile mipango ya Serikali ya muda mrefu na muda mfupi iweze kutekelezwa,” amesema.

Salome Makamba (Viti Maalum), alihoji muswada huo kutamka kuwa Rais atakuwa ndio mwenyekiti wa tume hiyo na wakati huo huo kuwa mshauri wa baraza mawaziri.

“Kama Rais alikuwa mwenyekiti waangeneza mipango wakaenda kwenye baraza kushauri maana yake kile kitu lazima kifanyike. Kwa mantinki hayo kama tume ya mipango kuna makosa ama kuna mambo madogo yantakiwa kurekbisha marekebisho baraza la mawaziri litakosa mamlaka ya kushauri,” amesema Makamba.