Muuguzi Hospitali ya Amana kortini tuhuma za kubaka, kulawiti mtoto

Muktasari:

  • Muuguzi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Amana jijini Dar es Salaam, Joseph Mwaipola (50) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu mashtaka matatu, yakiwemo ya kubaka na kulawiti mtoto wa miaka 17, ambaye alikuwa anamtibu.


Dar es Salaam. Muuguzi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Amana jijini Dar es Salaam, Joseph Mwaipola (50) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu mashtaka matatu, yakiwemo ya kubaka na kulawiti mtoto wa miaka 17, ambaye alikuwa anamtibu.

Mwaipola amefikishwa mahakamani hapo, leo Ijumaa Septemba 9, 2022 na kusomewa mashtaka yake na wakili wa Serikali Mwandamizi, Slyvia Mitanto mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Yusto Ruboroga.

Katika mashtaka yao, Mwaipola anadaiwa Februari 2022 katika Hospitali ya Rufaa ya Amana, iliyopo wilaya ya Ilala, alimbaka na kumlawiti binti wa miaka 17, kinyume cha sheria.

Pia, Mei 31, 2022 katika nyumba ya kulala wageni ya Pazuri Lodge iliyopo Temeke, jiji hapa, Mwaipola anadaiwa kumbaka binti huyo.

Upelelezi wa shauri hilo umekamilika na Hakimu Ruboroga ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 5, 2022, kesi hiyo itakapoitwa kwa ajili mshtakiwa kusomewa hoja za awali.