Muungano uligubikwa na siri, hofu

Muktasari:

  • Spika wa Bunge mstaafu, Pius Msekwa ameeleza jinsi Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar ulivyoingiwa kwa usiri kwa hofu ya kuingiliwa na maadui.


Dodoma/mikoani. Spika wa Bunge mstaafu, Pius Msekwa ameeleza jinsi Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar ulivyoingiwa kwa usiri kwa hofu ya kuingiliwa na maadui.

Hata hivyo, Msekwa amesema Muungano ni imara, utadumu zaidi na zaidi lakini akaonya kuwa “asiyeupenda akajinyonge.”

Mwanasiasa huyo mkongwe amesema kwamba jambo kubwa lililokuwa linatazamwa wakati huo ni usalama wa Zanzibar kutokana na tishio la waliopinduliwa kutaka kurudi tena.

Msekwa alitoa kauli hiyo jana, wakati akiwasilisha mada kwenye maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar jijini Dodoma.

Katika mada hiyo - Historia, chimbuko na misingi ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Msekwa alisema usiri ulikuwa mkubwa wakati wa majadiliano hadi kusaini mkataba wa Muungano baina ya Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume mjini Unguja.

“Jambo ambalo wengi hawalijui ni usiri mkubwa wa mazungumzo baina ya marais hao wawili walivyozungumza. Usiri mkubwa sana. Mazungumzo baina ya marais hao wawili kabla hawajakubaliana yaliendeshwa kwa siri kubwa. Sababu na umuhimu wa kuwepo kwa usiri huo ilikuwa ni hofu kubwa, kwamba endapo mazungumzo hayo yatajulikana mapema, basi maadui wanaweza wakatengeneza njama za kuhujumu jitihada hizo ili zisifikie lengo lake,” alisema.

Msekwa ambaye wakati huo alikuwa katibu wa Bunge, aliendelea kueleza namna Mwalimu Nyerere alivyopeleka muswada kwa haraka bungeni, ulivyopitishwa naye akausaini haraka. Vivyo hivyo kwa Zanzibar.

“Kwanza aliniagiza kuwa, wabunge wakiupitisha mara moja nimpelekee Ikulu. Nilifanya hivyo haraka na akasaini haraka nami nikiwa palepale, kwa kuwa ilikuwa ni jambo la haraka na dharura. Mara moja akafanya mawasiliano na mwenzake ambaye naye alikuwa amekamilisha huko (Zanzibar),” alisema Msekwa.

Aliwaeleza washiriki wa maadhimisho hayo kuwa siku ya kutia saini kabla hajasaini Mwalimu Nyerere aliomba glasi moja ya mvinyo kutokana na furaha aliyokuwa nayo, akanywa ndipo akasaini.

Alifafanua namna Nyerere alivyopeleka hoja hiyo na kupitishwa bila kupingwa chini ya usimamizi wa Rashid Kawawa siku ya Jumatatu Aprili 27, 1964 Bunge la Muungano lilipoitishwa.

Msekwa alisema kwa siku mbili za Bunge kulikuwa na kazi ya kuwateua na kuwaapisha wabunge wa Zanzibar na kazi nyingine ilikuwa ni kubadilishana hati za Muungano.

Msekwa aliyataja mambo matatu aliyosema kwamba yalisaidia kwenye chimbuko la Muungano ambayo ni haja ya kuulinda Muungano, utashi wa kisiasa na msingi wake ambao ulikuwa ni mapinduzi ya Januari 12, 1964.

Wengi hawaufahamu

Mapema akihutubia kongamano hilo la Muungano, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, alisema Watanzania wengi hawajui kuhusu umuhimu wa Muungano, hivyo iko haja ya kutoa elimu zaidi kuhusu faida zake.

Makamu wa Rais alisema ofisi yake itafanya juhudi hizo kupitia kitabu kilichoandikwa kuelezea mambo ya Muungano ili kiweze kuwafikia watu wengi wa Bara na Zanzibar.

Dk Mpango aliwaagiza watendaji katika ofisi yake Bara na Zanzibar kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kuhakikisha kitabu hicho kinawafikia wananchi, hususan vijana ili waweze kuufahamu na kuuelewa Muungano.

“Kwa takwimu zilizopo, Watanzani wengi wamezaliwa baada ya Muungano, kwa maana hiyo wanaufahamu kwa kuhadithiwa au kwa kusoma machapisho mbalimbali, hivyo hawana uelewa wa kutosha,” alisema Dk Mpango.

Alisema kitabu hicho pamoja na mambo mengine kinatoa tafsiri sahihi juu ya mambo ya Muungano, yalipotoka na wapi ulipo na unakoelekea, hatua ambayo itawawezesha Watanzania kuendelea kuuenzi zaidi.

Kwa mujibu wa Dk Mpango, kumekuwepo na mijadala mingi kuhusu historia, mantiki ya Muungano kwa nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar, faida na changamoto zake kwa lengo la kuendelea kujenga uelewa.

Hata hivyo, alisisitiza watu kuendelea kuulinda kwa kuwa una manufaa makubwa.

Baadaye akizungumza katika kongamano hilo, Waziri mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba alisema kwa sasa Muungano umeimarika zaidi kuliko ilivyokuwa kabla ya mwaka 1977, ambapo kulikuwa na matishio ya kutaka kuuvunja, hivyo anayo matumaini kuwa utadumu milele.

Jaji Warioba aliwataka viongozi kuacha kuzungumzia kero za Muungano kwa kuwa ni changamoto za kawaida na kila mahali zipo, hivyo umefika wakati wa kuzungumzia mambo yenye faida.

Mchangiaji mwingine, Ali Mzee alisema Watanzania wanajivuni Muungano huo ambao umewaweka pamoja na akaungana na Dk Mpango kuwa watu lazima waendelee kupewa elimu ya kutosha kuhusu faida zake.

Alieleza masikitiko yake kuwa kwa upande za Zanzibar waasisi wote wameshatangulia mbele za haki.

Mwinyi: Bila Muungano

Mjini Unguja Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alisema Tanzania bila Muungano ni jambo lisiloweza kufikiriwa, hivyo akawataka wananchi kuendelea kuuenzi na kuudumisha kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo.

Dk Mwinyi alitoa kauli hiyo Ikulu Zanzibar, katika salamu zake za kusherehekea miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

“Watanzania wengi wamezaliwa ndani ya Muungano, hivyo Tanzania bila Muungano ni kitu ambacho hakiwezi kufikiriwa, bado wananchi wake wapo pamoja na wataendelea kuwa wamoja,” alisema.

Dk Mwinyi alisema Muungano uliopo sasa ni wa damu zaidi kuliko wa vitu, maana wananchi wengi wana uhusiano kati ya Zanzibar na Tanzania Bara, hivyo wote ni wamoja.

Matukio mengine

Katika kusherehekea siku hiyo, mkuu wa Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, Halima Bulembo alisema kumbukumbu nzuri kwa wilaya hiyo kuadhimisha miaka 58 ya muungano ni kupanda miti.

Katika utekelezaji walipanda miche 600, lengo likiwa ni kupanda miti 1.5 milioni kwenye kata 37 za wilaya hiyo.

Mkoani Arusha Baraza la Wazee wa Chadema jimbo la Arusha walishauri kufanyika kwa maboresho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ili kuendelea kupunguza kero.

Mwenyekiti za Baraza hilo, Emmanuel Zakaria alisema ni muhimu kukaa chini na kutatua changamoto zilizopo ndani ya Muungano.

“Watanzania wengi bado tunauhitaji Muungano, lakini tunataka dosari zilizobainishwa mara kadhaa zifanyiwe kazi ili udumu,” alisema Zakaria.

Alisema Serikali irejee mapendekezo ya tume za majaji wastaafu Francis Nyalali, Robert Kisanga na Joseph Warioba ambao wamewahi kuzungumzia masuala ya Muungano.

Imeandikwa na Habel Chidawali na Sharon Sauwa (Dodoma), Jesse Mikofu (Unguja), Raisa Said (Muheza) na Mussa Juma (Arusha).