Muuza bucha amlaghai mwanafunzi kwa kumpa nyama, apata mimba

Lindi. Muuza nyama (buchani) Samwel Yohana Lindi mjini anatuhumiwa kumpa mimba mwanafunzi wa shule ya sekondari mwenye umri wa miaka 16.

Pamoja na serikali kufanya juhudi za kukabiliana na tatizo la wanafunzi wa kike kukatisha masomo kwa ajili ya mimba lakini hali bado sio nzuri kwa shule za sekondari mkoani humo.

Muuza nyama huyo inadaiwa amemshawishi mwanafunzi huyo kumpa nyama na kumsababishia kupata ujauzito uliomfanya ashindwe kuendelea na masomo bada ya uongozi wa shule kumsimamisha kwa mujibu wa sheria za shule.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Lindi, Ramadhani Dibelle amekiri kuwepo kwa matukio ya wanafunzi kupata mimba shuleni hapo.

"Tatizo hili lipo katika shule yangu kwani mwaka 2022/wanafunzi wawili, Amina Mpwawa na Nasra Hasani wamepata  mimba, mmoja kajifungua amerudi  darasani na kufanikiwa  kufanya mtihani  wa kidato cha nne na amepata daraja pili," amesema Divelle.

Amesema tatizo la mimba za wanafunzi linatokana na wazazi kukwepa majukumu na kuwaachia kina bibi na babu kulea watoto wao wakiwa wanahangaika na mambo mengine wakisahau malezi.

Mzazi wa Nasra Hasani amesema baada ya mtoto wake kubaini ana ujauzito alikimbia nyumbani kwake na kwenda kuishi kwa bibi.

Amesema kuwa baada ya kubaini mwanaye amepewa mimba na muuza nyama alifuata lakini mtuhumiwa alikuwa amekimbia, ndipo alipoamua kwenda kuripoti polisi lakini hakupata ushirikiano.

Nasra alipoulizwa kuhusiana na mimba hiyo, amesema amepewa na Samuel Yohona muuza nyama buchani.

"Mimba hii ya Samuel muuza nyama alikuwa ananipa nyama nikamkubali", amesema  mwanafunzi huyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Pili Mande alipoulizwa kuhusiana na matukio ya mimba yaliyoripotiwa,  amesema yapo lakini hawezi kutoa takwimu kwa kuwa yuko njiani.