Mvua yaua mwanafunzi Kibohehe
Muktasari:
Mvua hiyo iliyoandamana na upepo mkali iliangusha ukuta wa chumba cha darasa.
Mwanafunzi mmoja wa darasa la sita wa Shule ya Msingi
Kibohehe, iliyoko wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, amefariki dunia na
wengine watano kujeruhiwa, baada ya kuangukiwa na ukuta.
Mwanafunzi huyo wa kiume ameangukiwa na ukuta wa chumba cha
darasa baada ya mvua kubwa iliyoambatana na upepo kunyesha leo
mchana.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya Simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Kilimanjaro, Hamis Issah, amesema mwanafunzi huyo alikuwa akiingia
kwenye kipindi cha dini na ndipo alipokutana na ajali hiyo ya ukuta na
kupoteza maisha
“Mvua ilinyesha na upepo mkali, jengo moja la darasa likadondoka na
kumwangukia mtoto huyo ambaye alikuwa akiingia kwenye kipindi cha
dini,”amesema Issah.
Aidha Kamanda amesema, majeruhi wamepelekwa katika Hospitali ya Wilaya
ya Hai kwa ajili ya matibabu na kwamba uchunguzi zaidi wa tukio hilo
bado unaendelea.