Mvua zasababisha vifo 155, Majaliwa atoa maelekezo 14

Muktasari:

  • Waziri Mkuu amesema mvua za masika zimesababisha vifo 155, uharibifu wa mazao, makazi, mali za wananchi, miundombinu ya barabara, madaraja na reli.

Dar es Salaam. Mvua kubwa za El-Nino zilizoambatana na upepo mkali, mafuriko na maporomoko ya udongo katika maeneo mbalimbali nchini zimesababisha vifo vya watu 155 na wengine 236 kujeruhiwa.

Hayo yameelezwa bungeni leo Aprili 25, 2024 katika taarifa ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kuhusu changamoto za hali ya hewa nchini.

Amesema ongezeko la joto duniani limesababisha uwepo wa El-Nino ambayo imeambatana na mvua kubwa zilizosababisha mafuriko.

“Hapa nchini, mwezi Oktoba hadi Desemba 2023 kulikuwa na ongezeko kubwa la mvua ambapo jumla ya milimita 534.5 zilipimwa ikilinganishwa na milimita 227.2 kwa mwaka 2022 ikiwa ni ongezeko la asilimia 135. Vilevile, ongezeko hilo la mvua kubwa limeshuhudiwa katika kipindi cha mwezi Januari hadi Aprili 2024 na utabiri wa hali ya hewa unaonesha kuwa mvua za Masika zitaendelea hadi mwezi Mei, 2024,” amesema Majaliwa.

Waziri mkuu amesema mvua hizo zimesababisha uharibifu wa mazao, makazi, mali za wananchi, miundombinu kama vile barabara, madaraja na reli.

“Kutokana na athari hizo, zaidi ya kaya 51,000 na watu 200,000 wameathirika,” amesema.

Majaliwa amesema nyumba zaidi ya 10,000 zimeathirika kwa viwango tofauti.

“Maeneo mengine yaliyoathirika ni miundombinu ya shule, zahanati, nyumba za ibada, barabara, madaraja, mifugo na mashamba yenye mazao mbalimbali,” amesema.

Ameyataja baadhi ya maeneo yaliyoathirika nchini kuwa ni Rufiji na Kibiti mkoani Pwani, Malinyi, Mlimba, Kilosa, Manispaa ya Morogoro na Ifakara (Morogoro), Ilala, Kinondoni, Ubungo, Kigamboni na Temeke (Dar es Salaam), Same, Hai na Moshi (Kilimanjaro), Mbarali, Kyela na Halmashauri ya Jiji la Mbeya (Mbeya), Manispaa ya Kigoma Ujiji na Kakonko (Kigoma), Iringa Vijijini (Iringa), Manispaa ya Tabora (Tabora), Bahi (Dodoma), Lindi Manispaa, Kilwa, Liwale, na Nachingwea (Lindi), Masasi (Mtwara), na Jiji la Arusha, Monduli na Karatu (Arusha).

Mengine ni Muleba, Manispaa ya Bukoba (Kagera), Manispaa ya Shinyanga (Shinyanga), Geita Mji, Nyangh’wale na Chato (Geita), Mbozi na Momba (Songwe), Nkasi, Sumbawanga na Kalambo (Rukwa), Hanang’ (Manyara).

Waziri Mkuu amesema baadhi ya maeneo yaliyoathirika aliyatembelea na kujionea hali halisi.

“Hivi karibuni, mimi pamoja na mawaziri wanane wa kisekta tulitembelea maeneo ya Mlimba, Ifakara na Malinyi (Morogoro) na Rufiji (Pwani)” amesema.

Amewashukuru wadau mbalimbali nchini ambao wamekuwa mstari wa mbele kuungana na Serikali kuwasaidia Watanzania waliopatwa na majanga.

Majaliwa ametoa maelekezo 14 ya Serikali akiwataka wananchi kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.

“Ninawasihi sana wananchi kuwa na subira pindi wanapoona maji mengi yanapita hususan barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika,” amesema.


Maelekezo ya Serikali

1.   Taasisi za Serikali ziendelee, zijidhatiti kukabiliana na maafa kwa kushirikiana na wadau kutekeleza majukumu yaliyoanishwa katika Mpango wa Kujiandaa na Kukabiliana na Madhara ya El-Nino pamoja na mipango ya kisekta ili kuzuia na kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

2.   Kamati za Maafa za Wilaya na Mikoa ziendelee kuchukua hatua stahiki ikiwemo kutoa tahadhari kwa wananchi na kusaidia wananchi kwa wakati maafa yanapojitokeza.

3.   Niwasihi wananchi wafuatilie taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa na kuzingatia maelekezo yanayotolewa na viongozi katika maeneo yao, ikiwemo kuhamia maeneo salama, kulima mazao yanayopendekezwa.

4.   Wakuu wa mikoa na wilaya, maofisa tarafa, watendaji kata, mitaa na vijiji wasimamie ipasavyo usafi katika maeneo yao na kudhibiti utupaji taka ovyo unaosababisha kuziba kwa mitaro badala ya kusubiri usafi unaofanyika kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi.

5.   Kwa kuwa uharibifu wa mazingira umekuwa na athari kubwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi, viongozi wa ngazi zote washirikiane na wananchi kudhibiti uharibifu wa mazingira katika maeneo yao.

6.   Kwa kuwa Serikali imetoa maelekezo ya kufunga shule zilizoathiriwa na mafuriko, halmashauri na wamiliki wa shule zisizo za Serikali waweke utaratibu wa kufidia muda wa vipindi ili kukamilisha kalenda ya muhula kama ilivyopangwa.

7.   Wamiliki wa shule na madereva wa mabasi yanayotoa huduma za usafiri kwa wanafunzi wajiridhishe kuhusu njia wanazopita ili kuhakikisha usalama wa wanafunzi wanaowabeba katika vyombo vya usafiri.

8.   Wazazi, walezi na jamii ya Watanzania kwa ujumla washiriki kikamilifu katika kuhakikisha usalama wa wanafunzi wanapokwenda na kurudi shuleni wakati wote, hususan katika kipindi cha mvua.

9.   Wakala wa Barabara (Tanroads), Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), na mashirika ya reli (Tazara na TRC) wafanye tathmini ya barabara na njia za reli zilizoathirika na mafuriko kwenye maeneo mbalimbali na kuweka mpango wa kukarabati haraka ili kurejesha mawasiliano.

Aidha, wabainishe maeneo yanayopitiwa na mikondo ya maji kote na kuweka alama za tahadhari.

10. Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani liendelee kutoa tahadhari kwa madereva na watumiaji wengine wa barabara wakati wa mvua

11. Kamati za maafa katika ngazi za vijiji, wilaya na mikoa zisimamie kikamilifu ugawaji wa misaada inayotolewa kwa waathirika wa mafuriko na kuhakikisha kuwa misaada inawafikia walengwa.

12. Viongozi wa Serikali kuanzia ngazi ya vijiji wahamasishe na kuelimisha wananchi wanaoishi mabondeni kuhamia maeneo salama ili kuepusha maafa wakati wa mafuriko na kuhakikisha wanatenga maeneo salama yatakayotumika na wananchi watakaohamia kutoka mabondeni.

13. Mamlaka za mipango miji kote nchini zisimamie kikamilifu mipango miji ya halmashauri na kudhibiti ujenzi holela unaozuia njia za maji. Aidha, mipango ya matumizi bora ya ardhi iandaliwe katika maeneo yote ya vijiji na kusimamiwa ipasavyo.

14. Wizara ya Afya itoe elimu ya afya ya jamii ili kudhibiti magonjwa ya mlipuko pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa tiba.