Mvua zinavyoifanya Zingiziwa iwe eneo gumu la kuishi

Eneo la Daraja la Zingiziwa.

Muktasari:

  • Kufurika kwa maji katika Draja la Zingiziwa, wilayani Ilala kumesababisha wananchi washindwe kuvuka huku wengine wakilazimika kulipa Sh500 ili kuvushwa

Dar es Salaam. Licha ya uwepo wa Daraja la Zingiziwa katika Mtaa wa Zingiziwa wilayani Ilala, jijini Dar es Salaam safari ya kutoka mtaa huo kwenda mwingine imekuwa kikwazo.

Hiyo inatokana na mvua zinazoendelea kunyesha eneo hilo na mengine nchini, zilizosababisha daraja hilo kujaa maji na yanapita juu.

Kwa mujibu wa watumiaji wa daraja hilo, hali iliyopo sasa ni zaidi ya ile iliyokuwepo jana, huku Mamlaka ya Hali ya hewa Tanzania (TMA) ikitabiri kuendelea kwa mvua hizo hadi Jumapili ya Aprili 28, 2024.

Mwananchi Digital imeshuhudia wananchi wakipata tabu kuvuka katika eneo hilo, wengi wakishikwa mkono ili kuwaepusha wasisombwe na maji na kwa msaada huo walilazimika kuulipia Sh500.

Mbali na wananchi, maofisa wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) waliokuwa safarini kwenda kutengeneza transfoma iliyolipuka, nao walilazimika kuvushwa kwa utaratibu huo.

Hakuna gari wala pikipiki iliyokuwa inavuka katika eneo hilo, badala yake kila mwenye chombo chake cha usafiri aliishia kuiacha ng’ambo na kuvuka kwa mguu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika eneo hilo leo Ijumaa, Aprili 26, 2024 wananchi hao wamesema hali hiyo imekwaza shughuli zao.

Kujaa maji kwa daraja hilo, kulimlazimu Lulu Mkeni, mkazi wa Lukabaya kulipia Sh500 ili avushwe kwenda zilipo ofisi za mtendaji wa kata kupeleka barua ya maombi ya kazi.

"Serikali itengeneze eneo hili kwa kuwa kila mvua zikinyesha hali imekuwa ndio hii, hebu itimize ahadi yake nasi tupate ahueni, tunalazimika kuvuka kwa sababu tuna mahitaji upande wa pili,” amesema.

Hali hiyo ilikwamisha safari ya Mohammed Awadhi, dereva wa bodaboda kutoka Kariakoo, aliyekuwa na abiria wake anayepaswa kumpeleka nyumbani kwake ng’ambo ya daraja hilo.

"Inabidi tu nisubiri hadi maji yatakapopungua ili nimvushe mteja wangu yupo na mizigo mingi hawezi kuvuka nayo," amesema.

Kutokana na kujirudia kwa changamoto hiyo, Maria Makamburi anayetumia daraja hilo, amependekeza kujengwa kwa daraja kubwa zaidi.

Amesema changamoto zinazoendelea katika eneo hilo, zinasababisha hata wanafunzi washindwe kwenda shuleni.

Mwananchi mwingine, Halima Ramadhani amesema changamoto si daraja hilo pekee, hata barabara ni mbovu, akiisisitiza Serikali ifanye ujenzi.

Wengine furaha

Wakati wengine wakilalamikia madhila hayo, kwa baadhi ya vijana ilikuwa kicheko wakitaka Serikali iliache eneo hilo kama lilivyo.

Sababu ya tamanio lao hilo ni kile alichoeleza, wanajipatia fedha kwa kuvusha watu kutoka upande mmoja kwenda mwingine.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Zingiziwa, Mohamed Kirungi amesema tayari Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo alishafika kwenye eneo hilo kuona hali ilivyo.

“Tunaomba hatua zichukuliwe haraka,” amesema.