Mvutano Serikali, kanisa wachukua sura mpya Mbeya

Mchungaji kiongozi wa makanisa ya TCH -GOFN, John  Ikowelo akionyesha sehemu ya nyaraka za umiliki halali wa eneo ambalo Serikali imeweka zuio la ujenzi wa kanisa hilo katika eneo la Isanga Jijini Mbeya. Picha na Hawa Mathias

Muktasari:

  • Kanisa la TCH-GOFAN limo katika mzozo na Serikali ya Wilaya ya Mbeya baada ya kusitishiwa shughuli ya ujenzi wa Kanisa katika Bonde Ilolo ambalo inasema ni oevu na halifai kwa matumizi ya shughuli za kibinadamu wala makazi.

Mbeya. Waumini wa Kanisa la The Children of Gospel for Ally Nations (TCH-GOFAN) lililopo Wilaya ya Mbeya wamesema endapo Serikali wilayani hapa haitatoa kibali cha ujenzi wa kanisa lao watamchangia mchungaji wao kwenda kumuona Rais Samia Suluhu Hassan ili aweze kuingilia kati.

Hatua hiyo imekuja kufuatia kuwepo kwa mgogoro  uliodumu kwa zaidi ya miaka 20, baada ya Serikali kuweka zuio la uendelezaji wa makazi na kanisa katika Bonde la Ilolo, ambalo linaelezwa kuwa kwenye mkondo wa maji.

Akizungumza na waandishi habari leo, Jumapili Desemba 24, 2023, Mchungaji kiongozi wa Makanisa  ya TCH-GOFAN, John Ikowelo amesema  wamevumilia kwa  takribani miaka 20 lakini hawajui hatima yao, licha ya kufuatilia hatua kwa hatua kwa viongozi wa Serikali, akiwemo mkuu wa wilaya hiyo.

“Hilo eneo lipo jirani na Shule ya Msingi Isanga, ni mali ya kanisa lakini cha kushangaza baada ya mgogoro ya awali kuisha, wakati tumeanza kumwaga mawe, mchanga na  hatua za kuchimba msingi tumeletewa barua ya kuwekewa zuio,” amesema.

Mchungaji Ikowelo amesema hatua hiyo imewashangaza, licha ya kuwa wavumilivu na  kutumia busara, hivyo amewataka viongozi wa Serikali  kuwa hofu ya Mungu kwa kutenda haki.

Amesema kwa sasa hawako tayari kuendelea kupoteza muda, wanasubiri kauli ya mwisho ya mkuu wa wilaya ili kuchukua hatua ya kwenda kuonana na Rais Samia.

“Tumechoka kuzungushwa, kama kanisa tulitumia busara kuanzia ngazi za chini za viongozi wa Serikali lakini hawaoni hilo, si kwamba tumeshindwa  kumuona Mbunge Dk Tulia Ackson na Mkuu wa Mkoa, Juma Homera ila hatutaki kuwatwisha mzigo ambao umeshindwa kutatuliwa na watu walio chini yao,” amesema.

Mmoja wa waumini wa kanisa hilo, Enelise Kyanula amesema waumini walichanga mawe, mchanga na nguvu kazi kwa ajili ya kuanza ujenzi lakini cha kushangaza wameletewa barua ya zuio.

“Kwa sasa tumefika wakati tumechoka tunaendelea kuomba na kulia tu, kinachofuata ni kujichanga ili kiongozi wa kanisa akaonane na Rais Samia aweze kuingilia kati haki itendeke, tujenge nyumba ya  bwana,” amesema.

Akizungumzia suala hilo, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa amesema kama Serikali haitaweza kutoa kibali cha ujenzi kwa sababu ni eneo oevu, eneo hilo halitaruhusiwa kuwekezwa mradi wowote.

“Nilipofika Mbeya nimeukuta mgogoro huo, nimefika eneo linalolalamikiwa nimeongea na viongozi wa kanisa, kimsingi nimepewa maelezo na Mkurugenzi wa Jiji na watu wa ardhi kuwa halistahili kujengwa kwa sababu ni oevu,”amesema Malisa.

Amesema kuwa kama Serikali sasa wanaangalia ni wapi halmashauri itapata eneo la wazi na kulikabidhi kanisa hilo kwa ajili ya ujenzi.

Kuhusu kuwekeza pale, haitowezekana na endapo hawataridhia, waendelee na hatua nyingine kama  vile kwenda mahakamani.