Mwakilishi Mtambwe kuanzisha mfuko wa dharura

Mwakilishi wa Jimbo la Mtambwe kutoka Chama cha ACT-Wazalendo Dkt.Mohamed Ali Suleiman akila kiapo cha utiifu ndani ya Baraza la wawakilishi Chukwani Zanzibar. Picha na Muhammed Khamis

Muktasari:

  • Mwakilishi Mtambwe Dk Mohamed Ali Suleiman, anakusudia kuanzisha mfuko maalumu wa dharura kwa wananchi wa jimbo hilo, sambamba na kuandaa maandiko ya miradi ya maendeleo kwaajili ya kutafuta wafadhili huku akisema Serikali peke yake haiwezi kutatua changamoto zote kwa wananchi.

Unguja. Mwakilishi jimbo la Mtambwe, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Dk Mohamed Ali Suleman ameapa rasmi kuwa Mwakilishi wa jimbo hilo huku akiahidi kusaka wadau mbalimbali kwa ajili ya kuchochea maendeleo jimboni humo.

Dk Suleman ameapishwa leo, Jumatano, Novemba 29, 2023 katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani nje kidogo ya Mji wa Unguja ambapo Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid ndiye aliyongoza shughuli hiyo iliyofanyika katika siku ya kwanza ya kikao cha 13 cha baraza hilo.

Kuapishwa kwa Mwakilishi huyo kumekuja baada ya kufanyika kwa uchaguzi mdogo Oktoba 28 mwaka huu uliompa ushindi wa kura zipatazo 2449 dhidi ya mpinzani wake wa CCM Hamad Khamis aliepata kura 1531.

Uchaguzi huo mdogo ulifanyika baada ya aliyekuwa Mwakilishi wa jimbo hilo kupitia ACT Wazalendo, Habib Mohammed Ali kufariki dunia Ijumaa Machi 3, 2023.

Leo wakati akienda kuapishwa Mwakilishi huyo, alisindikizwa barazani hapo na viongozi na wanachama wa ACT-Wazalendo wakiambatana na familia, huku Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Bimani akiongoza msafara huo.

Mara baada ya kula kiapo, mwakilishi huyo amezungumza na Mwananchi Digital katika viunga vya baraza hilo na kuahidi  kuwa atatumia nafasi hiyo kuwatetea wananchi wa jimbo lake ili waweze kuwa sawa kimaendeleo na wananchi wa maeneno mengine.

Amesema anafahamu kuwa Serikali haiwezi kufanya shughuli zote za kimaendeleo peke yake hivyo atatumia nafasi hiyo kuandikia miradi mbalimbali na kuomba ufadhili kutoka kwa mashirika tofauti.

‘’Kwa mfano baada ya wiki moja nitarudi Pemba kuzindua rasmi mfuko wa dharura wa jimbo, ambao utafanya kazi za kuwasaidia wananchi wa jimboni, hasa wale wanaopata matatizo na kuhitaji msaada wa haraka,” amesema.

Akizungumiza kuhusu mfuko huo amesema unalenga kuwasaidia akinamama wajawazito wanaohitaji huduma za haraka kwa lengo la kuokoa maisha ya mama na mtoto.

Amesema kupitia utafiti aliofanya amebaini katika jimbo hilo kumekuwepo na changamoto ambazo zinaweza kutatuliwa, iwapo kutakuwa na na mipango madhubuti ambayo yeye anakwenda kuitekeleza kwa faida ya wananchi wote.

Amesema atatumia vyema fursa ya kuwa mwakilishi japo kwa kipindi kifupi kilichobaki kupambania maeneo yote ndani ya jimbo hilo ambayo mpaka sasa bado hayana umeme na huduma ya maji safi na salama kwa muda mrefu.