Mwalimu jela miaka 30 kwa kubaka

Saturday June 12 2021
kubaka pc
By Mary Mwaisenye

Chunya. Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela mwalimu wa Shule ya Sekondari Isangawana, Dotto Salandi (33) kwa kosa la kumbaka mwanafunzi wa shule hiyo mwenye umri wa miaka 17 (jina limehifadhiwa).

Imedaiwa na Mwendesha mashtaka wa Jamhuri, Damas Chonya mbele ya Hakimu John Msafiri katika kesi ya jinai 84/2021, Salandi alikutwa akifanya mapenzi na mwanafunzi huyo katika nyumba ya mwalimu Samson Njonanje ambaye naye anatuhumiwa kumbaka mwanafunzi na kumsababishia ujauzito.

Alidai kosa hilo ni kinyume cha sheria ya makosa ya jinai namba 130(1)(2)(e) na 131(1) sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019.

Shahidi wa kwanza ambaye ni mzazi wa mtoto aliiambia mahakama kuwa mwanawe alifanyiwa ukatili na mwalimu Dotto, taarifa alizopata kutoka uongozi wa Tarafa kutokana na malalamiko ya wazazi juu ya walimu wa Isangawana.

Upande wa Jamhuri umeleta mashahidi watano, akiwemo mwanafunzi aliyebakwa ambaye aliiambia mahakama kuwa mwalimu Dotto alimbaka ndipo alipokutwa na kutimua mbio uchi bwenini huku akiziacha nguo za shule ambazo zililetwa mahakamani kama ushahidi.

Shahidi mwingine ambaye ni daktari aliyempima mwanafunzi huyo alidai mwanafunzi alibakwa na alitoa PF 3 iwe kielelezo.

Advertisement

Upande wa Jamhuri ulimleta Ofisa Tarafa ya Kipembawe alidai kuwa kikao cha wazazi kilichohudhuriwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mayeka Simon Mayeka kilibaini baadhi ya walimu hujihusisha mapenzi na wanafunzi, akiwemo Dotto ambaye ni miongoni mwa walimu waliopigiwa kura.

Shahidi huyo aliiambia mahakama kuwa siku ya tukio alikwenda kushuhudia namna mwalimu alivyokamatwa na zoezi la utambuzi wa nguo za mwanafunzi huyo ambapo upekee aliouona ni alama katika sweta, ambayo ilitambuliwa na wanafunzi.

Shahidi mwingine ambaye ni askari aliyemkamata mtuhumiwa aliiambia mahakama kuwa walipata taarifa na walipofuatilia walikumkuta mwalimu akifanya mapenzi na mwanafunzi.

Kwa upande wake, Mwalimu Dotto Salandi aliyekuwa anatetewa na wakili Stewart Ngwale alikana kutenda kosa hilo.

Salandi alimleta shahidi mmoja mwalimu Samson Njonanje aliiambia mahakama kuwa mwalimu huyo amesingiziwa tu.

Advertisement