Mwalimu mbaroni kwa kumjeruhi mwanafunzi

Mwalimu mbaroni kwa kumjeruhi mwanafunzi

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, linamshikilia mwalimu mmoja wa Shule ya Msingi Majengo, Manispaa ya Moshi, kwa tuhuma za kumshambulia mwanafunzi wa darasa la tano na kumsababishia majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili wake.

Moshi. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, linamshikilia mwalimu mmoja wa Shule ya Msingi Majengo, Manispaa ya Moshi, kwa tuhuma za kumshambulia mwanafunzi wa darasa la tano na kumsababishia majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili wake.

Tukio hilo linadaiwa kutokea Oktoba 15, 2021, shuleni hapo baada ya mwanafunzi huyo kushindwa kukamilisha kazi aliyokuwa amepewa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa akizungumza leo Jumatatu Oktoba 18, 2021 amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa mwalimu huyo ambaye jina linahifadhiwa, wanamshikilia.

"Ni kweli tukio hilo lipo, mwalimu tayari tumemkamata tunamshikilia na tunaendelea kumuhoji, tunasubiri afisa ustawi wa jamii afike, ili mtoto aweze kuhojiwa,"amesema kamanda Maigwa.

Akizungumza mama wa mtoto huyo, Rose George amesema mtoto wake huyo ameshambuliwa vibaya kwa kupigwa ngumi, fimbo na mateke mwilini na mwalimu wake huyo baada ya kushindwa kumaliza kazi ya hisabati aliyokuwa amepewa.

"Niligundua tatizo la mwanangu kuumizwa, baada ya mtoto kupata homa kali usiku, nilimpa Panadol lakini haikushuka, asubuhi niliamka kumuandaa ili nimpeleke hospitali, ndipo nikamkuta na majeraha mbalimbali mwilini,"

"Nilimuuliza akasema mwalimu alimpiga kwa kuwa alikuwa hajamaliza kazi ya hisabati na alimtishia asiseme na mtoto akaogopa kusema,"amesema.