Mwalimu Mkuu mbaroni akidaiwa kumpa mimba mwanafunzi wake

Mwalimu mbaroni kwa kumjeruhi mwanafunzi

Muktasari:

  • Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi, Kilimo wilayani Misungwi mkoani Mwanza, Charles Maige anadaiwa kumbaka mwanafunzi huyo zaidi ya mara tatu hadi kumpatia ujauzito na hivyo kumkatisha masomo yake.

Mwanza. Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kilimo wilayani Misungwi mkoani Mwanza, Charles Maige anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa tuhuma za kumbaka na kumpa ujauzito mwanafunzi wa darasa la saba (jina limehifadhiwa) katika shule hiyo.

Wengine wanaoshikiliwa ni Mwalimu, Venance Komba anayedaiwa kumshurutisha mwanafunzi huyo ampe (tendo) ili asitoe siri na Mwenyekiti wa Kamati ya Shule hiyo, Isack Kubini anayedaiwa kuifuata familia ya mtoto huyo kwa lengo la kutaka suala hilo limalizwe nyumbani.

Akisimulia alivyofanyiwa ukatili huo mwanafunzi huyo (15) amesema; "Ilikuwa siku ya Jumamosi mwalimu alipita maeneo ya nyumbani na kunikuta nikfua, aliniambia natembea mwanafunzi wangu upo hapo unafua, chukua hii hela (Sh500) ukaninunulie ‘super glue’ dukani,” amesema.

Ameongeza; "Baada ya kununua hiyo ‘super glue’ niliipeleka nyumbani kwa mwalimu mita chache kutoka nyumbani kwetu, na kumkuta akiwa ameketi ndani, nilisita kuingia ila akanilazimisha kuingia ndani, na baadaye kuniingilia kimwili huku akinionyesha kisu na kunitishia kuwa nikisema ananichinja."

Mlezi wa mwanafunzi huyo, Restuta Theophili alisema Juni 18 mwaka huu alibaini kuwa mtoto huyo huenda akawa na ujauzito baada ya kuona akisuasua kufanya kazi na kusinzia mara kwa mara anapokuwa nyumbani.

"Nilivyoona mambo siyo mazuri nikaenda kumchukua kipimo bila kumwambia nafanya kitu gani nilivyopima nikaona kipimo kimeonyesha ana ujauzito. Nikakaa naye kisha nikamwambia twende dukani tukaondoa tukapitia huko kwenda hadi kituo cha Polisi Usagara," amesema.

Amesema kituoni aliandikiwa PF3 kisha kupelekwa Kituo cha Afya Idetemya wilayani humo ambapo nako majibu ya vipimo yalionyesha ana ujauzito usiopungua miezi miwili.

Kufuatia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Misungwi mkoani hapa, Paulo Chacha ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani humo amefika katika shule hiyo na kuagiza mkuu huyo wa shule akamatwe.

Paulo amesema pamoja na kuwa ni tuhuma analitaka Jeshi la Polisi kutompatia dhamana mwalimu huyo kwa kile alichodai kumekuwa na mfululizo wa matukio ya baadhi ya ndugu na marafiki wanaodaiwa kutumia fedha kupoza suala hilo.

Paulo amesema mbali tukio hilo, amepokea malalamiko ya wazazi wa wanafunzi wawili wakidai watoto wao kulazimishwa kufanya ngono na mwalimu huyo huku akionya kuwa hatofumbia macho suala hilo.

"Hata kama ni tuhuma, anatuhumiwaje mwalimu mkuu kumpa mtoto mimba? Hao wengine wawili nao wanamtuhumu mwalimu huyo huyo kwa kuwashika matiti huku akiwaita 'mchumba wangu' ukinikataa mimi utapata shida," amesema.