Mwalimu Mtanzania awania tuzo ya ubora duniani

Mwalimu wa Shule ya Sekondari Kiara Manispaa ya Musoma mkoani Mara, James Kidiga

Dar es Salaam. Mwalimu wa Shule ya Sekondari Kiara Manispaa ya Musoma mkoani Mara, James Kidiga ni miongoni mwa walimu 50 wanaowania tuzo ya mwalimu bora duniani.

Kidiga ambaye ni mwalimu wa Kiingereza ndiye mwalimu pekee kutoka Tanzania anayewania tuzo hiyo itakayotolewa Ufaransa Novemba mwaka huu.

Jina la Kidiga limetangazwa hivi karibuni kupitia tovuti ya tuzo za walimu duniani ‘Global teacher prize 2023.’

Tuzo hizo zimeandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) kwa kushirikiana na Taasisi ya Varkey Foundation.

Akizungumzia hatua hiyo kwa simu na Mwananchi juzi, Ofisa Elimu Mkoa wa Mara, Makwasa Bulenga alisema taarifa hizo wamezipokea kwa furaha kwani ni heshima kwa mkoa huo.

“Hii inaonyesha kuwa tuna walimu wenye uwezo hata kuzidi nchi ambazo wanaona elimu yao iko juu kuzidi elimu ya Tanzani,” alisema Bulenga.

“Tukiwajenga walimu wetu katika mazingira mazuri ya ufundishaji basi tuna walimu wenye uwezo wa kufundisha na kujulikana duniani,”alisema.

Bulenga alisema Mwalimu Kidiga amekuwa akijitolea kufundisha walimu wenzake Kiingereza na ni mfano bora kwa walimu wenzake mkoani humo.

Mwalimu Kidiga ambaye ni mratibu wa Chama cha Walimu wa Kiingereza Mara, aliliambia Mwananchi juzi kuwa, zaidi walimu 7,000 waliomba nafasi hiyo kutoka nchi 130 duniani.

“Hii ni fursa ambayo huwa inatangazwa kila mwaka, niliomba na nikafanyiwa usahili nikapita, washindi hutangazawa kuanzia nafasi ya 50 hadi nafasi ya kwanza, mshindi wa kwanza anapata Dola 1 milioni za Marekani ( Sh2.5 bilioni), mpaka sasa bado tupo kwenye mchujo kumpata mshindi wa kwanza,” alisema mwalimu Kidiga.

Pia, alisema katikati ya Oktoba, watatangazwa walimu walioshika nafasi ya kwanza mpaka ya 10 na kusafirishwa kwenda ufaransa kwa ajili ya tuzo.

“Napenda kuhamasisha walimu wenzangu kuchangamkia fursa mbalimbali licha uwepo wa changamoto wenye mazingira yetu ya kazi, hizi zitatusaidia kufahamiana na wenzetu na kubadilishana uzoefu,”alisema.

Akitangaza wateule hao, Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa Unesco idara ya Elimu, Stefania Giannini alisema, “Napenda kutoa pongezi zangu za dhati kwa washiriki wote waliofika fainali.

“Unesco ni mshirika wa kujivunia wa tuzo ya walimu duniani, kwa sababu walimu wanastahili kutambuliwa. Juhudi zao zina jukumu kubwa katika kubadilisha elimu kwa siku zijazo,"alisema.

Agosti 2022, mwalimu Kidiga alikuwa miongoni mwa walimu wanne walioalikwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda baada ya kushinda programu ya kujenga ustadi na umahiri wa walimu kwa miezi sita inayoandaliwa na ubalozi wa Marekani (Fulbright Tea).