Mwanafunzi afariki kwa kupigwa na radi, mwalimu ajeruhiwa

Thursday April 15 2021
mvua pc
By Alodia Dominick

Bukoba. Mwanafunzi wa kidato cha nne Shule ya Sekondari Kabugalo,  Gisera Oswardi (18) amefariki  kwa kupigwa na radi huku mwalimu wa shule hiyo, Charles Alphonce akijeruhiwa.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Alhamisi Aprili 15, 2021 Alphonce  amesema tukio hilo limetokea leo saa 3 asubuhi na kwamba walipigwa na radi wakati wanatoka darasani kwenda ofisini.

“Wakati natoka darasani naelekea ofisini nikiwa nimejifunika mwamvuli nimeongozana na Gisera nilisikia moto nikaanguka chini na kuanzia kiunoni kushuka miguuni nilikuwa kama nimepigwa ganzi, muda si mrefu walifika walimu kutupeleka hospitali,” amesema.

Mganga mkuu mfawidhi hospitali ya rufaa Mkoa wa Kagera, Mselata Nyakiroto amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akibainisha kuwa alipokea taarifa ya majeruhi mmoja na maiti moja waliopigwa na radi.

“Hadi wanafika hospitali mwanafunzi alikuwa ameshafariki na mwalimu alikuwa na majeraha miguuni na kwenye mikono, amepatiwa matibabu anaendelea vizuri.”

“Uchunguzi wa awali umeonyesha kifo cha mwanafunzi kimetokana na radi kumuunguza sehemu kubwa za mwili wake,” amesisitiza.

Advertisement

Ndugu wa mwanafunzi huyo, Adinani Said amesema mazishi ya ndugu yao yatafanyika kijiji cha Ibosa halmashauri ya Bukoba.

Advertisement